Thursday, March 9, 2017
RAIS MUTHARIKA KUHOJIWA BUNGENI
Do you like this story?
BUNGE
la Malawi liko katika mchakato wa mabadiliko ya kanuni zake ili pamoja
na mambo mengine, liweze kumwita na kumhoji Rais wa nchi hiyo,Profesa
Peter Mutharika, kujibu maswali kadhaa yanayohusu mwenendo wa nchi hiyo
pale inapolazimu.
Lakini si tu
Mutharika ambaye kwa sasa ndiye yupo madarakani na ni kama vile
mabadiliko hayo yanamlenga moja kwa moja, bali hata marais wengine
watakaomfuatia baada ya kustaafu kwake, nao pia watalazimika kufika
bungeni kwa ajili ya kuhojiwa kwa kadiri Bunge hilo la Malawi
litakavyoamua kuhusu kuendelea na kanuni zake hizo mpya.
Mapendekezo
ya mabadiliko ya kanuni yamewasilishwa katika Bunge la nchi hiyo na
Kamati ya Mambo ya Sheria ya Muhimili huo na katika kanuni husika,
itawekwa bayana siku na muda ambao mkuu wa nchi atafika bungeni kwa
ajili ya shughuli ya mahojiano.
Katiba
ya Malawi chini ya kifungu chake namba 89 (4) inaeleza kwamba rais
anapaswa kwenda bungeni kwa ajili ya kipindi cha kujibu maswali ya
wabunge tu na sasa kanuni zinarekebishwa ili aweze kuitwa hata nyakati
nyingine kwa kadiri masuala mazito ya kitaifa yatakavyokuwa
yakijitokeza.
Mwenyekiti wa kamati hiyo
ya Bunge, Maxwell Thyolera, amezungumzia hatua hiyo akisema kwamba
wamependekeza kanuni mpya ili kumleta rais bungeni kwa ajili ya muda wa
maswali siku ya Jumatano na hata ikibidi mara kwa mara kwa kadiri ya
makubaliano ya wabunge.
Thyolera
alisema rais atatakiwa kujibu si zaidi ya maswali matano katika kila
kikao atakachoitwa. “Muda wa kumuuliza maswali rais itakuwa ni saa moja
na dakika thelathini,” alisema Thyolera.
“Kuongeza
muda wa maswali haitaruhusiwa, kulingana na kanuni namba 68 (kifungu
cha 5 na 6). Hata hivyo, maswali matano ya nyongeza katika maswali ya
msingi yataruhusiwa lakini hayatatumika katika kujumuisha masuala ambayo
hayapo kwenye maswali ya msingi,” alifafanua
Tofauti
na kipindi ambacho mawaziri hujibu maswali kutoka kwa wabunge, rais
ataheshimiwa na atalindwa, kanuni hiyo mpya imebainisha.
Kwa
sasa, kanuni inamruhusu rais aliyeko madarakani kumpa waziri wake
yeyote kazi ya kujibu maswali yanayoelekezwa kwake katika siku za
Jumatano.
Mutharika amewahi kufanya
hivyo mara mbili kwa kiongozi wa Bunge kujibu maswali ambayo mengi
yalikuwa yametolewa na kiongozi wa upinzani bungeni Lazarus Chakwera.
Rais
wa zamani Bakili Muluzi alikabiliana na kiongozi wa upinzani wa wakati
huo, Gwanda Chakuamba, bungeni katika muda uliosisimua katika historia
nchini humo miaka ya 1990.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS MUTHARIKA KUHOJIWA BUNGENI”
Post a Comment