Thursday, March 9, 2017
TAARIFA TOKA CHAMA CHA WANANCHI CUF
Do you like this story?
THE CIVIC UNITED FRONT
CUF-CHAMA CHA WANANCHI)
TAREHE: 08/03/2017
MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
(PRESS CONFERENCE)
TAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MUENDELEZO WA HUJUMA NA NJAMA ANAZOFANYA IBRAHIMU LIPUMBA NA WASHIRIKA WAKE DHIDI YA CHAMA CHA CUF NA VIONGOZI WAKE KWA KILE ALICHOKIITA KUTENGUA UTEUZI WA WAKURUGENZI NA MANAIBU WAKURUGENZI.
TAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MUENDELEZO WA HUJUMA NA NJAMA ANAZOFANYA IBRAHIMU LIPUMBA NA WASHIRIKA WAKE DHIDI YA CHAMA CHA CUF NA VIONGOZI WAKE KWA KILE ALICHOKIITA KUTENGUA UTEUZI WA WAKURUGENZI NA MANAIBU WAKURUGENZI.
Ndugu Waandishi wa Habari,
(Assalamu aleykum)
Awali
ya yote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia
uhai na Afya njema tukaweza kukutana wakati huu kwa ajili ya kuzungumza
nanyi. Niwashukuru kwa kuitikia wito wetu wa kuja kutusikiliza na
kupitia kwenu kuzungumza na watanzania wote waliopo ndani na nje ya nchi
yetu. Tuwashukuru kwa ushirikiano munaoendelea kukipa chama chetu cha
CUF mara zote kwa kujulisha Wananchi kwa usahihi masuala mbalimbali
yanayoendelea na hasa katika kipindi hichi ambacho kwa makusudi na
dhamira ovu dhidi ya Chama. Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji
Francis Mutungi ametupandikizia mgogoro usiokuwepo hapo kabla wa
kulazimisha kutaka kutuchagulia viongozi wa Taasisi yetu kinyume na
kazi, wajibu na majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa
Sura ya 258, iliyoanzisha uwepo wa Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa
nchini.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Tarehe 4/3/2017 mimi
binafsi na wenzangu ambao ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa
tulipokea ujumbe mfupi (SMS) wenye maudhui yanayofanana katika simu zetu
unaoeleza kuwa; Mheshimiwa Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui,
Muheshimiwa Salim Bimani- Mkurugenzi wa Habari na Uenezi na Mawasiliano
na Umma. Mhe. Abdalla Bakar Hassan – Naibu Mkurugenzi wa fedha na
Uchumi. Mhe. Omar Ali Shehe – Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi.
Mhe. Pavu Juma Abdallah – Naibu Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu
na Mhe. Yussuf Salim Hussein – Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Mhe.
Mahmud Mahinda – Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana Taifa, Ujumbe
huoukieleza kuwa na tunanukuu.
“Nimeagizwa na Mkt Taifa kuandaa
kikao cha Kamati Tendaji Taifa. Kitakachofanyika tarehe 6/3/2017 ofisi
kuu Buguruni saa 3.00 asbh….Katika kikao hicho Mkt atahudhuria ana
maswala muhimu ya kuongea na wajumbe….Tafadhali unaombwa kuhudhuria bila
ya kukosa….NMKB.. Magdalena Sakaya”mwisho wa kunukuu. Ujumbe huo
tumeujibu kwa barua yenye Kumb Na. CUF/HQ/AKM/003/017/03 ya tarehe
5/3/2017 na kusainiwa na sisi sote na kuituma barua hiyo kwa njia ya
email yasakayamagdalena@gmail.com
Jumapili majira ya saa 4 usiku na nakala halisi za barua hiyo tumeituma
Dar es Salaam Jana tarehe 6/3/2017 wakala wa mahakama (Court Broker)
ameendelea na taratibu zake za kufikisha barua hiyo rasmi kwake. Nakala
ya barua hiyo nimeiambatanisha na taarifa hii.
Jana tarehe
6/3/2017 Magdalena Sakaya na Lipumba wameshindwa kufanya kikao
walichokiita cha Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa kuwa hakukuwa na
wajumbe halali waliohudhuria kikao hicho lakini pia hakukuwa na akidi
iliyotimia hata ya hao wajumbe ‘Fake’ waliohudhuria. Badala yake na kwa
kuwa alikuwa anajua anguko hilo alishafanya maandalizi ya kuwaita
waandishi wa habari na kufanya mkutano ambao alitangaza kwa kile
alichokiitaKUTENGUA UTEUZI WA WAKURUGENZI NA MANAIBU WAKURUGENZI WOTE
KWA UPANDE WA ZANZIBAR kwa madai ya mamlaka aliyopewa na Katiba ya CUF
pamoja na kutoonesha ni Ibara ipi hiyo ya Katiba iliyompa mamlaka hayo
ya kutengua uteuzi wa Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi ambao majina
yao nimeyaorodhesha hapo juu.
Akieleza sababu za kufanya hivyo
kuwa eti wameshindwa kuhudhuria kikao kilichoitishwa na Magdalena Sakaya
kwa agizo lake. Lipumba anadai eti ameamua kufanya hivyo kwa kuwa
Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad hafiki Ofisi Kuu Buguruni ili ampe
maelekezo ya ujenzi wa Chama na mipango ya kuimarisha Chama na
kukabiliana na matatizo na Changamoto za Chama. Na kwamba alitaka kutoa
muongozo kwa kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya Taifa juu ya mambo
aliyoyaita muhimu ya kuandaa kama ajenda za kufikishwa kwenye Baraza
Kuu. Mambo hayo ni pamoja na;
a) Utekelezaji wa Maamuzi ya
Baraza Kuu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 October 2015
kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar;
b)
Tathmini ya Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani; (c) Mkakati wa Chama wa
kukabiliana na hali ya kisiasa ya Zanzibar; (d) Tathmini ya Uchaguzi
Mdogo wa madiwani katika kata 20 za Tanzania Bara; (e) Mpango Mkakati wa
Ujenzi wa Chama Tanzania Bara; (f) Kupitia Bajeti ya Chama ya 2016/17
na maandalizi ya bajeti ya 2017/18.
Ndugu waandishi wa habari,
The
Civic United Front (CUF –Chama Cha Wananchi) ikiwa ni Taasisi imara
yenye maamuzi na misimamo isiyoyumba wala kuyumbishwa na yeyote awaye,
ikiongozwa na Jemedari wa mapambano ya Kudai Mamlaka Kamili, Haki, Usawa
na Neema kwa wote Maalim Seif Sharif Hamad, inapenda kutoa ufafanuzi wa
masuala hayo na kuweka msimamo wake kama ifuatavyo;
1. Kama
tulivyoeleza hapo juu ni kweli tulipokea ujumbe mfupi (SMS) kwenye simu
zetu kutoka kwa Magdalena Sakaya tarehe 4/3/2017 majira ya saa 6 za
usiku na tumemjibu kwa barua yenye maelezo yanayojitosheleza kwamba;
“Hatukuona uhalali wa kikao hicho ulichotutaka tuhudhurie. Kikao hicho
si halali kwa mujibu wa Katiba ya CUF Itakuwa ni haramu na makosa
makubwa kwetu kuwajibika kwa mamlaka zisizo na mamlaka kisheria na ki
Katiba. Kikao hicho ni BATILI Hatuwezi kuwa sehemu ya washiriki wa
kutaka kukihujumu Chama chetu cha CUF na kwa mantiki hiyo,HATUTOHUDHURIA
kikao hicho”.
2. Kwa mujibu wa Katiba ya CUF Ibara ya 84 (1)
ikisomwa pamoja na Ibara ya 93 (1)(d) inaeleza kuwa; “Kutakuwa na Kamati
ya Utendaji ya Taifa ambayo itakutana mara moja kwa kila miezi miwili.
Isipokuwa kwamba ikitokea dharura Kamati hiyo inaweza kufanya kikao cha
dharura wakati wowote ambao Mwenyekiti wa Kamati hiyo ataamuru hivyo.”
Mwenye mamlaka ya KUAMURU kuitishwa kwa Kamati ya Utendaji ya Taifa ni
Mwenyekiti wa kamati hiyo ambae ni Katibu Mkuu ambaye yupo Ofisini Makao
makuu Mtendeni, Zanzibar na anaendelea na anatekeleza majukumu na
wajibu wake kama Katiba inavyomtaka kufanya hivyo. Sote ni mashahidi
kuwa hivi karibuni tarehe 24/2/2017 amekamilisha ziara ya kikazi ya
ukaguzi na Uimarishaji wa Chama aliyoifanya katika wilaya zote za Unguja
na Pemba.
3. Maalim Seif amepata mapokezi makubwa yenye hamasa
na shauku, imani na mapenzi ya dhati ya wananchi juu yake. Maalim Seif
ameweza kufungua ofisi mpya za matawi na majimbo, kumbi za mikutano,
amezindua waratibu wa Chama zaidi ya 1600, amepokea wanachama wapya
waliojiunga CUF, na kufanya vikao na viongozi wa kada mbalimbali za
Chama. Kwa mara ya mwisho ameongoza kikao cha kawaida cha Kamati ya
Utendaji ya Taifa kilifanyika tarehe 2/2/2017 katika ofisi ndogo ya
Chama Vuga, Mjini Unguja.
4. Magdalena Sakaya amechukuliwa
hatua za kinidhamu na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa katika kikao chake
kilichofanyika tarehe 28/8/2016 katika Ofisi ya Makao Makuu ya Chama
Vuga, Mjini-Unguja. Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 46 halali kati
ya wajumbe wote 59.
Wajumbe walifikia maamuzi ya kumsimamisha
uanachama. Maamuzi hayo ya kusimamishwa uanachama hakuridhika nayo na
kwa mujibu wa Katiba ya CUF Ibara ya 108 (5) ameamua kukata Rufaa kwa
Mkutano Mkuu wa Taifa kwa barua yake ya tareh 5/9/2016 na kupokelewa
Ofisi kuu Buguruni Tarehe 11/9/2017. Ibara hiyo inaeleza “Mwanachama au
kiongozi yeyote aliyeamua kukata Rufaa kwa jambo lolote lile, basi
atafanya hivyo kwa ngazi iliyo juu ya kikao kilichotoa maamuzi ambayo
hakuridhika nayo katika kipindi kisichozidi siku kumi na nne (14) tokea
siku ulipotolewa uamuzi huo”. Kwa maamuzi hayo ya Baraza Kuu, Magdalena
Sakaya si Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara.
5. Baraza Kuu
la Uongozi la Taifa kwa mamlaka yake ya Kikatiba Ibara ya 97 (4)
(kuhusu kusimamishwa/kufukuzwa uongozi Naibu Katibu Mkuu) ikisomwa
pamoja na Ibara ya 105(1) (kuhusu kukaimu madaraka) imemteua Mheshimiwa
Joran Lwehabura Bashange kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara.
Ibara hizo zinaeleza kama ifuatavyo; “Endapo Naibu Katibu Mkuu
ataachishwa au kufukuzwa uongozi, basi Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
litamchagua mwanachama mwengine kujaza nafasi hiyo kwa mujibu wa
masharti ya Katiba hii” Ibara ya 97(4)
“Pale ambapo mwanachama
yeyote wa chama mwenye madaraka kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii,
kwa sababu yeyote ile, hawezi kutekeleza kazi zake kwa muda au
amesimamishwa au kuvuliwa madaraka kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii,
mamlaka iliyo na uwezo wa uchaguzi au uteuzi wa nafasi hiyo inaweza
kumteua mwanachama mwingine mwenye sifa zinazohitajika kukaimu madaraka
hayo”. Ibara 105 (1)
6. Ibrahim Lipumba alijiuzulu nafasi ya
uenyekiti wa Chama Taifa kwa matakwa yake mwenyewe binafsi. Alikataa
katakata ushauri wa kutochukua maamuzi hayo. Baraza Kuu likaandaa ajenda
na kuitisha Mkutano Mkuu Maalum/dharura wa Taifa uliofanyika katika
Hotel ya Blue Pearl Tarehe 21/8/2016 na wajumbe 476 kati ya wajumbe 700
wa Mkutano huo waliohudhuria walikubali kujiuzulu kwake kama Ibara ya
117 (2) inavyoelekeza.
Kutokana na Lipumba kuvamia Mkutano Mkuu
huo bila kualikwa, kusababisha vurugu na uharibifu wa mali, samani za
Hotel na kukisababishia Chama hasara ya kiasi cha shilingi milioni 600
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa katika kikao chake kilichofanyika tarehe
28/8/2016 kilifikia maamuzi ya kumsimamisha UANACHAMA Lipumba, na baadae
Tarehe 24/9/2016 alifanya uvamizi wa Ofisi Kuu ya Chama Buguruni akiwa
na kundi la wahuni na kufanya uharibifu wa mali na thamani pamoja na
kuwajeruhi wanachama na walinzi wa Ofisi.
Kutokana na vitendo
hivyo vya ukiukaji wa Katiba ya Chama, utovu wa nidhamu na kukiharibia
chama taswira yake mbele ya jamii, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa katika
kikao chake cha tarehe 27/9/2016 lilifikia maamuzi ya KUMFUKUZA
UANACHAMA. Lipumba si Mwenyekiti wala mwanachama wa CUF. Hana mamlaka ya
kuagiza kufanyika kwa kikao chochote kile cha chama, kuteua na au
kutengua watendaji wa Chama.
7. Lipumba amekuwa msahaulifu
sana. Katika taarifa yake ameeleza kuwa tangu tarehe 23/9/2016 amekuwa
akitoa wito kwa Katibu Mkuu, Maalim Seif aende ofisini Buguruni ili ampe
maelekezo ya Mipango ya ujenzi wa Chama. Lipumba amesahau kuwa wakati
huo Katibu Mkuu alikuwa anaendelea na majukumu yake katika Ofisi hiyo ya
Buguruni.
Lipumba na wahuni wenzake wamefanya uvamizi wa ofisi ya
Chama Buguruni siku ya Jumamosi ya Tarehe 24 Septemba, 2016. Na Tangu
wakati huo Chama kupitia Bodi ya Wadhamini ya CUF imefungua shauri la
madai Namba 23/2016 mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Msajili
wa Vyama vya siasa nchini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Lipumba na
wenzake wengine 10 ili kupata tafsiri ya kisheria juu ya uhalali wa
maamuzi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi
kuingilia shughuli za utendaji wa Chama na maamuzi halali ya vikao
vyake. Shauri bado linaendelea Mahakamani na limepangwa kutajwa tarehe
22/3/2017.
8. Tunashindwa kumuelewa Lipumba anaposema ameagiza
eti kufanyika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa lengo la
kuzungumzia ujenzi wa Chama na mipango ya kuimarisha Chama. Anataka
kujua Utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza Kuu baada ya Uchaguzi Mkuu wa
Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar, Mkakati wa Chama wa kukabiliana na hali ya kisiasa
ya Zanzibar, Kupitia Bajeti ya Chama ya 2016/17 na maandalizi ya bajeti
ya 2017/18 Hili nalo linastaajabisha kwa sababu Lipumba si Mwanachama
wa CUF, ameshafukuzwa UANACHAMA. Uwepo wake CUF mpaka sasa unatokana na
njama na hila za Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya siasa nchini
wa kutoheshimu sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa ofisi yake
na Vyombo vya dola kumlinda kwa amri ya viongozi wa CCM.
Kiongozi
gani wa CUF atakaye kuwa tayari kukaa meza moja na Lipumba kuzungumzia
eti mipango ya ujenzi wa Chama hali ya kuwa Lipumba amekuwa swahiba
mkubwa wa Viongozi wa CCM na serikali yake? Kila uchao haishi kufanya
vikao vya siri na viongozi hao? Viongozi wa CCM Tanzania Bara na
Viongozi wa CCM Zanzibar, nani atamwamini kibaraka Lipumba aliyekubali
kutumiwa? Mkakati gani wa Chama wa kukabiliana na hali ya kisiasa
Zanzibar unaoweza kujadiliana na kupanga na Lipumba hali ya kuwa tarehe
10 februari, 2017 alikuja Zanzibar kwa kificho na kukutana na Viongozi
wa CCM kupanga kufanya haya anayoendelea kuyafanya sasa?
9.
Tangu ajiuzulu Baraza Kuu la uongozi la Taifa limefanya vikao vyake vya
kikatiba na kujadili masuala mbalimbali na limefikia maazimio ya msingi
kwa mustakbali mwema wa CUF, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Hatuna
jambo jipya ambalo tunahitaji kuelekezwa kulijadili na au kulipanga kwa
maelekezo ya Lipumba. Lipumba anazungumzia eti kupanga bajeti ya chama
2016/2017 na maandalizi ya bajeti ya chama ya mwaka 2017/18. Lipumba
amechanganyikiwa? Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limepanga Bajeti ya
Chama katika vikao vyake vilivyofanyika mwaka jana 2016. Lipumba
ameshirikiana na Jaji Francis Mutungi kuiba fedha za ruzuku ya chama
kinyume na Katiba ya CUF na taratibu za Chama kiasi cha shilingi milioni
369.
Lipumba amegawana fedha hizo na washirika wake aidha wiki
kadhaa zilizopita waliomba kupatiwa tena kiasi cha shilingi milioni 230
fedha za ruzuku za CUF kama walivyofanya awali. Hawakufanikiwa,
wamekutana na vikwazo vilivyowekwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF kutokana
na wizi walioufanya awali kutoka kwa mamlaka za usimamizi wa fedha hizo
serikalini. Je wakati huo hakuona umuhimu wa kuitisha Kikao cha kupanga
bajeti ya chama kama yeye anadai ni Mwenyekiti Halali wa chama na ana
nia njema na chama cha CUF
10. Hata kama angekuwa ni Mwenyekiti
Halali wa Chama Taifa, Lipumba hana mamlaka ya kuwachukulia hatua za
kinidhamu watendaji wa Chama. katika dhana ya uwajibikaji na mizania ya
utendaji haki, usawa na usimamizi bora(Check and Balance) na mgawanyo wa
madaraka (Separation of Power)Mwenyekiti wa Chama amepewa mamlaka ya
Kuteua watendaji kwa mujibu wa Ibara ya 90 (1) (f) inayoeleeza kuwa;
“Atateua kutoka miongoni mwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, Wajumbe
wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, au wanachama wajasiri wa Chama,
Wakurugenzi na Manaibu wakurugenzi wa Kurugenzi za Chama Kitaifa, Katibu
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Taifa na Naibu Katibu wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama, baada ya kushauriana na Makamu Mwenyekiti, na
kufikisha uteuzi wake huo mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa
kuthibitishwa. Ila ijulikane kuwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na
wanachama wajasiri wa Chama walioteuliwa kuwa Wakurugenzi/Manaibu
Wakurugenzi, Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Naibu Katibu wa
Ulinzi na Usalama ambao hawakuwa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa kabla ya kuteuliwa kushika nyadhifa hizo watasita kuwa Wajumbe wa
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa mara tu baada ya kusita kushika nyadhifa
hizo.”
Hakuna Ibara yeyote ya Katiba ya CUF inayompa mamlaka
kuwatengua Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi na Viongozi wengine wa
Chama. Ibara ya 85 (11) (kuhusu Wajibu wa Kamati ya Utendaji ya Taifa)
“Kumsimamisha kazi Mkurugenzi na Naibu Mkurugenzi kwa utovu wa nidhamu
au kushindwa kazi na kulitaarifu Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa
uamuzi wa mwisho” Baraza Kuu la CUF ndio muhimili wa usimamizi wa
shughuli za Chama
Ibara ya 113 (1) (imeeleza kuhusu masharti ya kuchaguliwa na kipindi cha uongozi)
“Isipokuwa
pale ambapo Katiba hii imeeleza vinginevyo masharti ya kuchaguliwa kwa
kiongozi na kipindi cha uongozi kitakuwa kama hivi:- “Kipindi cha
uongozi wa chama kitakuwa miaka mitano (5) kwa ngazi zote isipokuwa kama
kiongozi huyo ameshindwa kazi aliyopewa” Kama kumetokezea suala lolote
lile la kinidhamu na maadili lilipaswa kupita katika mkondo huu wa
kiKatiba. Lipumba amekurupuka. CUF ni taasisi Imara sio kikundi cha
wahuni kama Lipumba na genge lake wanavyojidhihirisha. Lazima utaratibu
wa kikatiba ulipaswa kuzingatiwa pale ambapo kama angekuwa na mamlaka
halali ya kufanya alivyofanya. Pindi panapotokea utovu wa nidhamu na
ukiukwaji wa maadili ya uongozi Katiba ya Chama imeweka kamati maalumu
ya kushughulikia Nidhamu na Maadili. Kamati hiyo inaongozwa na Makamu
Mwenyekiti wa Chama. Ibara ya 92 (c), 99 (1) (2) na 100 (1) (2) (3) (4)
(Ibara na vifungu hivi vinazungumzia Kamati ya Maadili na Nidhamu,
Wajumbe wa Kamati na majukumu yake)
Lengo la kunukuu maelezo haya
ya Katiba ni kuonyesha kuwa Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi na Katibu
Mtendaji wa JUVICUF aliodai Lipumba kuwatengua hawajashindwa kutekeleza
majukumu yao, Watendaji hao wote wamekuwa mstari wa mbele katika
mapambano ya kukiletea ushindi chama chetu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015 Oktoba 25, 2015 na kupelekea kuwagaragaza vibaya CCM kwa kura
nyingi na Maalim Seif Sharif Hamad Kushinda nafasi ya Urais wa Zanzibar.
Lipumba hana msingi wa uhalali wa maamuzi yake (Basis of Justification)
zaidi ya chuki, kutumika, na ukibaraka wa kutaka kurudisha nyuma juhudi
za kuwaletea Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla Mamlaka Kamili, Haki,
Usawa Na Neema kwa Wote. Watendaji hawa wanalindwa na Katiba ya Chama na
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
11. Kutokana na Makamu Mwenyekiti
wa CUF Mhe. Juma Duni Haji kujiuzulu mwaka 2015 kwa madhumuni ya
kujenga nguvu ya pamoja ndani ya UKAWA na kuchaguliwa kuwa mgombea
mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015 ikizingatiwa maslahi mapana ya kitaifa, hakika huo ulikuwa
mkakati na maamuzi sahihi (Executive and Strategic Decision) ambao
mpaka sasa CUF na viongozi wake wote makini wanauheshimu uamuzi huo. CUF
inaongozwa na Kamati ya Uongozi Taifa iliyoundwa na Baraza Kuu la
Uongozi Taifa kwa mujibu wa Katiba ya CUF Ibara ya 101 (1) (kuhusu
Baraza Kuu la uongozi la Taifa Kuanzisha Kamati/ Taasisi za Kitaifa)
“Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linaweza, pindi likiona inafaa kuanzisha
Kamati, Tume au Taasisi yoyote ile ya Kitaifa yenye lengo la kusaidia
utekelezaji mzuri wa sera na itikadi za Chama, au kufanya uchunguzi juu
ya jambo lolote lile linalohitaji kufanyiwa uchunguzi”.
Kamati
hiyo ya Uongozi Taifa inaongozwa wajumbe watatu (3) na Mwenyekiti wake
Mhe. Julius Mtatiro, Saverina Mwijage (MB), na Katani Ahmed Katani (MB)
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa wanaotambuliwa na kuthibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama ni
1. Maalim Seif Sharif Hamad -Mwenyekiti
2. Joran Lwehabura Bashange -Kaimu Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi
3. Nassor Ahmed Mazrui -Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar Zanzibar
4. Abdallah Khamis – Naibu Mkurugenzi wa fedha na Uchumi
5. Mustafa Wandwi -Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama
6. Yussuf Salim – Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama.
7. Umar Ali Sheikh – Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi
8. Shaweji Mketo – Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi
9. Ismail Jussa Ladhu -Mkurugenzi wa mambo ya nje na Mahusiano ya Kimataifa.
10. Abdallah Mtolea – Naibu Mkurugenzi wa mambo ya nje na mahusiano ya Kimataifa
11. Salim Bimani – Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma.
12. Mbarala Maharagande – Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma.
13. Kulthum Mchuchuri -Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu.
14. Pavu Abdallah – Naibu Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu.
15. Mahmoud Ali Mahinda, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana Taifa-JUVICUF
16. Fatuma Kalembo- Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wanawake Taifa-JUKECUF
17. Na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wazee wa Taifa -CUF-JUZECUF
Mwisho:
Tunawata
wanachama, wapenzi wa CUF na viongozi wetu wote kutokuwa na wasiwasi
wowote kwa kadhia hii inayoendelea kufanywa na vibaraka wa CCM. Tembeeni
kifua mbele macho mita mia moja kwa kujiamini kabisa. CUF ni taasisi
imara yenye viongozi makini. Katiba ya CUF inatambua kuwepo kwa Kamati
ya Utendaji ya Taifa Moja pekee na wajumbe wake ni hao tuliowataja hapa.
Hakuna na wala hakutakuwa na Kamati ya Utendaji nyingine. Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa lipo na limeendelea kukutana kama kawaida. Bodi ya
Wadhamini ya CUF ipo na imefanya maamuzi mengi muhimu na ya msingi
kukilinda Chama chini ya Mwenyekiti wake Mhe.Abdallah Khatau na hivi
karibuni ndio imeamuru kufungwa kwa akaunti zote za CUF ili zisiendelee
kutumiwa na Lipumba na genge lake kufanya uhalifu wa kuiba fedha za
Chama za Ruzuku.
Tunatoa pongezi kubwa kwa wanachama na viongozi
wetu wa Mkoani Tanga kwa kumkataa na kumpuuza Lipumba na wenzake
waliokwenda mkoani humo kwa ziara ya kutaka kukivuruga Chama. Bodi ya
Wadhamini ya CUF imefungua kesi ya madai kuwazuia kutekeleza majukumu ya
Chama wale wote waliochukuliwa hatua za kinidhamu na Chama na waliopewa
nafasi za uongozi na mtu asiyekuwa na mamlaka hayo katika mahakama ya
Kisutu Dar es Salaam na leo baadae tutawajulisha maamuzi ya maombi hayo
yaliyowasilishwa mahakamani hapo. Itakumbukwa kuwa CUF imevuka vigingi
vizito katika nyakati tofauti kila ilipojaribiwa ikiwa kwa uadui wa
ndani au wa nje. Na kwa ithibati, dhati na imani kubwa ni kwamba mwisho
wa vitimbi hivi vyote, CUF itaibuka mshindi. Tunatoa wito kwa wanachama,
wapenzi wa CUF, na watanzania wote kwa ujumla wapenda mabadiliko,
waendelee kuwa na Subira na kila mmoja atekeleze wajibu wake kikamilifu
katika eneo lake.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
HAKI SAWA KWA WOTE
NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU-ZANZIBAR
IMETOLEWA LEO TAREHE 8/3/2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TAARIFA TOKA CHAMA CHA WANANCHI CUF”
Post a Comment