Sunday, March 19, 2017

TRAFIKI MBEYA WALALAMIKIWA KUNG`OA NAMBA ZA MAGARI KWENYE MAEGESHO


Polisi wa Usalama Barabarani Jijini Mbeya wakitoa namba za Magari ambayo yameendeshwa pembezoni mwa barabara ya( LUPA WAY) iliopo katikati ya Jiji(Picha na David Nyembe wa Fahari News Mbeya)

Mwonekano wa Baadhi ya Magari ambayo yametolewa namba katika Eneo la Uwindini Jijini Mbeya(Picha na David Nyembe wa Fahari News Mbeya)



Mbeya.Wakazi wa jiji la Mbeya wamelalamikia vitendo vinavyofanywa  na Askari wa Usalama Barabarani  vya  kung`oa namba za usajili za magari yaliyoegeshwa katika mtaa wa Lupa (LUPA WAY)huku  madereva wake wakiwa hawapo.

Wakizungumza na Fahari News kwa nyakati tofauti walisema kuwa eneo ambalo wameegesha magari hayo hakuna alama yoyote ambayo inazuia kufanya hivyo na kwamba ni muda muda mrefu sehemu hiyo imekuwa ikitumika kuegesha magari.


Alisema kama jiji  imeona kuna umuhimu wa eneo hilo lisitumike kwa ajili ya maegesho ya magari wangetoa tangazo au kuweka vibao ambavyo vinaonyesha kuwa hilo siyo eneo la kuegesha magari.

“Tunachokiona kama wananchi ni kwamba trafiki wameona watumie njia hiyo kukusanya fedha za haraka haraka kwani hakuna taarifa yoyote ambayo imetolewa na wala alama maalum kama ilivyo kwa maeneo mengine ambayo yanakatazwa  kuegesha magari”alisema Wiliam John

John alisema katika majiji mengi yanakuwa na utaratibu wake kwani wanakuwa wametenga maeneo kwa ajili ya maegesho ya magari na yale ambayo hayatakwi kuna alama  yakikutaka  usioegeshe gari katika eneo hilo.

Ofisa habari wa jiji la Mbeya John Kiluwa alisema amepokea malalamiko hayo tangu juzi  kutoka kwa wananchi na kwamba amefanyia kazi lakini kama halmashauri ya jiji hakuna taarifa yoyote kuhusiana na zoezi hilo.

"Nimepokea malalamiko hayo tangu juzi kutoka kwa watu mbali mbali hivyo na kama halmashauri hatuna taarifa yoyote kuhusiana na zoezi hilo na hatujui ni kwa sababu gani wameamua kufanya hivyo labda uwatafute wenyewe jeshi la polisi wakueleze  kwa ni ni wameamua kufanya hivyo."alisema

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Dhahiri Kidavashari alisema hana taarifa yoyote kuhusiana na zoezi hilo na kuahidi kulifuatilia kwa wahusika ili kujua ni kwa sababu gani wameamua kung`oa namba kwenye magari ya watu ambayo yameegeshwa katika eneo hilo.

Mwisho.

0 Responses to “TRAFIKI MBEYA WALALAMIKIWA KUNG`OA NAMBA ZA MAGARI KWENYE MAEGESHO”

Post a Comment

More to Read