Wednesday, April 19, 2017

AUDIO; SIKILIZA HAPA BINTI ANAYEDAIWA KUFA PAPO HAPO KWA KUGONGWA NA GARI AONEKANA MAKABURINI AKIWA HAI


BINTI anayejulikana kwa jina la Anna Mathew (18), mkazi wa Mbezi Juu, eneo la Gold Star Jijini Dar es Salaam, aliyedaiwa kugongwa na gari na kufariki dunia papo hapo eneo la Tangi Bovu Barabara ya Bagamoyo, majira ya saa 11 alfariji wakati akitokea katika starehe usiku wa kuamkia Jumatatu ya pasaka ameonekana makaburini akiwa hai.
Habari za binti huyo kufariki zilifika kwa familia yake kutoka kwa mwendesha Bodaboda mmoja aliyeshuhudia ajali hiyo na kumtambua marehemu huyo ambaye alisema gari iliyomgonga haikusimama.
Wakisimulia zaidi mashuhuda wa tukio hilo lililowashangaza wengi walisema baada ya ajali walimfunika na khanga yake ilIyokuwa katika mkoba wake huku wakisubiri askari kufika eneo la tukio kwa ajili ya taratibu pamoja na kuchukua mwili.
''Majira ya saa kumi na mbili walifika polisi na kuchukua mwili huo kisha kuupeleka hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kuhifadhiwa na kusubiri taratibu za maziko'',alisema shuhuda mmoja.
Alisema baada ya wanafamilia kupata taarifa hizo walijikusanya na kwenda hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kujiridhisha na kuutambua mwili.
Akizungumzia tukio hilo mama mkubwa wa Anna, aliyejitambulisha kwa jina la Ester Joseph alisema walipofika hospitalini hapo alishindwa kuitambua maiti iliyodaiwa ni ya binti yao kutokana na mwili huo kuvimba.
''Polisi tuliokuwa tumeongozana nao walianza kunifokea kwamba inakuwaje nashindwa kumtambua mwanangu? Mimi kwa kweli nilikuwa hata simuelewi vizuri sikuweza kumtambua kwani alikuwa amevimba uso, hadi askari walianza kunifokea hivyo nikatoka nje lakini alipokwenda baba yake mzazi alimtambua na kutoa jibu kwamba aliyemuona ndiye hasa mwanawe na alipoulizwa alisema kuwa alimtambua kupitia miguu'',alisema Ester.
''Baba mzazi na kaka wa Anna walipoingia walimtambua na kuthibitisha kuwa waliyemuona mahala hapo alikuwa ni Anna, kisha tukaondoka kurudi nyumbani kuendelea na taratibu na maandalizi ya maziko, ambapo ilipangwa azikwe leo Jumanne",aliongeza.
Kama ilivyo kawaida ya msiba majirani walikusanyika na kufanya taratibu zinazotakiwa kufanywa ikiwa ni pamoja na kuchangisha fedha kwa ajili ya matumizi katika msiba huo,huku wengine wakifunga Maturubai na akina mama wakiwasha moto kuandaa chakula.
Majira ya jioni majirani walikusanyika kama ilivyo kawaida ya msiba mara alifika kijana mmoja msibani hapo aliyetambuliwa kwa jina la Anuary ambaye ni dereva wa bodaboda na pia ni mganga wa jadi ambaye hafahamiki zaidi kwa kazi hiyo mtaani hapo.
Wakisimulia majirani walisema kuwa kijana huyo alipofika alianza kupaza sauti na kuwataka majirani kutawanyika kwamba hapakuwa na msiba mahala hapo na kuwataka kutokula chakula cha msiba.
Kijana huyo aliteua wazee wawili waliotajwa kwa majina, Mzee Super na Abdallah Mlali, ili waondoke wote kuelekea alipo binti huyo aliyewekewa matanga kuwa amefariki.
Imeelezwa kuwa baadhi ya watu walianza kumpinga na kumdharau wakidhani kuwa alikuwa amelewa na akitania, huku wengine wakimfukuza msibani hapo.
Kijana huyo aliondoka na mzee mmoja kati ya hao waili, Mzee Super na kwenda naye hadi makaburini ambako walimkuta Anna akiwa hawezi hata kuzungumza na kijana huyo alipandisha Mashetani na kuanza kumfuata binti huyo na kumkamata na kisha kuondoka naye hadi katika nyumba ya jirani na msiba huo.
Baada ya kufika naye Mzee Super alikimbia kwenda kutoa taarifa kwa wanandugu kuwa binti yao ameonekana akiwa mzima, jambo ambalo liliwashangaza wanandugu na kuzuka taharuki kubwa mahala hapo huku kila mmoja akiwa haamini kinachosemwa, baadhi ya ndugu waliondoka na kwenda kuthibitisha na kumkuta akiwa na mganga huyo huku akiwa hawezi kuzungumza.
Wanandugu walirudi nyumbani na kukaa kikao huku wakiwa bado hawaamini kile walichokiona wakifananisha na sura ya mwili waliuona chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mwananyamala.
Baada ya tukio hilo wanandugu walikubaliana na kumwachia kijana huyo aendelee na kazi ya kumzindua, huku akiwa amepandisha mashetani na baadaye aliomba kwa wananchi waliokuwa wamefurika nje ya nyumba hiyo kumletea kuku mweupe ama mwekundu, jambo lililotekelezwa kwa haraka na majirani hao ambapo dereva mmoja wa bodaboda alijitolea kumfuata kuku wake Goba na kumleta mahala hapo ili binti afanyiwe dawa hiyo.
Hatimaye Binti alizinduka na kuanza kuongea huku akiwatambua baadhi ya watu akiwemo mama yake mzazi, Elizabeth Joseph, akimkumbatia huku akibugujikwa na machozi, shangwe nderemo na vifijo vikitawala mahala hapo, kutoka kwa wananchi waliofurika eneo hilo na kila mmoja akisema yake.
''Wanga wa Mbezi Juu mmeshindwa leo, mlizoea kutufanya mandondocha na kutuulia ndugu zetu leo mmekutana na mbabe wenu'' walisikika baadhi ya wananchi wakisema kwa sauti.
Akizungumza na mtandao huu baada ya kazi hiyo nzito, Kijana Anuary alisema baada ya kupata taarifa ya msiba huo, aliamua kumpigia simu babu yake anayeishi jijini Tanga na kumfahamisha mlolongo mzima wa tukio, lakini babu yake alimwambia kuwa hapakuwa na msiba na wala binti huyo hajafariki na kumpa maelekezo jinsi ya kumpata akiwa hai.


Alisema na ndipo alipata ujasiri baada ya maelekezo hayo aliyafanyia kazi, kama alivyowahi kufanya siku za nyuma mtaani hapo na kufanikisha kumkamata mzee aliyekuwa akiwatesa wakazi wa mtaa huo kwa kuwalawiti kimazingara, ambaye aliamua kuhama na kukimbia nyumba yake kwa aibu, kutokana na jinsi alivyokuwa akiogopwa mtaani hapo.
Akisimulia mkasa huo baada ya tukio hilo, Anna alisema kuwa siku ya sikukuu ya Pasaka, aliondoka nyumbani kwao majira ya jioni kuelekea katika 'Birthday' ya rafiki yake akiwa na rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Salma.
Alisema baada ya kumalizika kwa sherehe hiyo walirejea nyumbani na mwenzake ambaye aliingia ndani na yeye kuingia chooni kujisaidia na wakati akiwa chooni, alisikia sauti ikimuita jina lake na akaitika akijua aliyekuwa akimwita ni Salma, ambapo alisema kuwa baada ya hapo hakujua tena kinachoendelea hadi asubuhi alipojikuta akiwa makaburini.
''Nilipokuwa makaburini, nilikuwa nikiwaona watu ninaowajua, ndugu zangu wakipita lakini nilikuwa ninawaita wao hawanisikii wala hawanioni, nilikuwa hata sijielewi hata nielekee wapi wala hata njia ya kutoka pale siioni, na hadi najikuta hapa nikiwa nimezungukwa na watu kama hivi'' ,alisema Anna.
Naye kijana aliyeshuhudia ajali hiyo alisema alishtushwa na taarifa hizo za kuonekana binti huyo akiwa mzima kwani alishuhudia binti huyo akifunikwa khanga yake mwenyewe na kubebwa na gari  la polisi akiwa amefariki.

0 Responses to “AUDIO; SIKILIZA HAPA BINTI ANAYEDAIWA KUFA PAPO HAPO KWA KUGONGWA NA GARI AONEKANA MAKABURINI AKIWA HAI”

Post a Comment

More to Read