Friday, April 28, 2017
MFANYABIASHARA WA KUKU ADAI ALISINGIZWA KESI YA MAUAJI KISA ANA VVU ASIWAAMBUKIZE
Do you like this story?
MFANYABIASHARA
wa kuku, Michael Gadi (52) amedai kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji cha
Ngulu Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro walimsingizia kesi ya mauaji
baada ya kushindwa kumfukuza kwa kuhofia atawaambukiza Virusi Vya Ukimwi
(VVU).
Gadi alieleza hayo juzi mbele ya Jaji Patricia Fikirini wakati
akijitetea dhidi ya mashitaka ya mauaji ya bila kukusudia yanayomkabili
katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.
Akitoa ushahidi wake huku akiongozwa na Wakili Elikunda Kipoko, Gadi
alidai kwa muda mrefu wanakijiji walikuwa wanafanya njama za kumuondoa,
kwa sababu asiwaambukize VVU.
Wakili Kipoko: Mshitakiwa, kesi inayokukabili inasema ulimuua Michael Masanga kwa kumchoma kisu, ni kweli? Gadi: Siyo kweli
Wakili Kipoko: Unaieleza nini mahakama kuhusu tuhuma hizo? Gadi:
Sijafanya hilo kosa, unajua kijijini tunaishi kwa wivu na kwa muda
mrefu, walikuwa wanafanya njama za kuniondoa kwa sababu ya maradhi yangu
(VVU) wanaona nitawachafulia kijiji.
Katika utetezi wake, Gadi alidai kuwa Mei 18, 2014, alitoka Same na
kurudi nyumbani saa 10 jioni, akapumzika ilipofika usiku alisikia
kelele, akafungua dirisha na kuona watu wengi pamoja na askari wa mgambo
wakimtaka afungue mlango lakini alikataa kufanya hivyo hadi balozi
atakapofika.
Aliendelea kudai baada ya balozi kufika alifungua mlango na askari
walimkamata na kukagua ndani kwake, wakachukua kisu na kumpeleka katika
kituo kidogo cha polisi cha Ngulu na baadaye alihamishiwa kituo cha
Mwanga.
Gadi alidai baada ya siku tatu walimtoa kituoni na kumueleza wanakwenda
nyumbani kwake kukagua tena, walipofika akawaambia hawezi kufungua
mlango kwa sababu askari anayeitwa Samweli alichukua ufunguo wa nyumbani
kwake.
Alidai walimtafuta askari Samweli akawafungulia mlango “wakati
wakiendelea kukagua nilisikia wakisema kisu hiki hapa kwenye godoro,
wakaniuliza hiki kisu cha nani? nikawaambia siyo changu wamuulize
aliyekuwa na ufunguo wa chumba changu”.
Katika ushahidi wake Gadi alikana maelezo aliyoyatoa kituo cha polisi
pia alidai hajawahi kuzungumza na Masanga (marehemu) zaidi ya kujua jina
lake.
Baada ya kusikiliza ushahidi huo, Jaji Fikirini aliahirisha kesi hiyo
hadi leo kwa ajili ya pande zote mbili kuwasilisha majumuisho ya hoja,
upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi saba na mshitakiwa alijitetea
mwenyewe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MFANYABIASHARA WA KUKU ADAI ALISINGIZWA KESI YA MAUAJI KISA ANA VVU ASIWAAMBUKIZE”
Post a Comment