Friday, April 28, 2017

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA ASHAURIWA NA LHRC




Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, LHRC, kimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuhakikisha ustawi mzuri wa vyama vya siasa kwa kutatua migogoro iliyopo ndani na baina ya vyama vya siasa ili kuepusha matukio ya uvunjifu wa amani.

Aidha LHRC, kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Dk. Hellen Kijo Bisimba, kimesema vyama vya siasa vinapaswa kutumia uhuru wao kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa bila kusababisha uvunjifu wa amani.

Kauli ya kituo hicho imetolewa kulaani tukio la uvamizi katika mkutano wa ndani wa Chama cha Wananchi (CUF) uliosababisha kupigwa na kujeruhiwa kwa wanachama na waandishi wa habari huko Mabibo, Ubungo, Dar es Salaam ambalo limezidi kuzua mjadala katika jamii kuhusu hatma ya hali ya usalama kwa taifa.

Dk. Kijo Bisima amesema, tukio hilo ni ukiukwaji mkubwa wa misingi ya demokrasia kwa kuzingatia aina ya shughuli iliyokuwa ikiendelea na kwamba, tukio hilo pia limezua hofu kuhusu usalama wa wanahabari wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao jambo ambalo linazorotesha haki ya kupata taarifa.

0 Responses to “ MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA ASHAURIWA NA LHRC”

Post a Comment

More to Read