Tuesday, April 18, 2017

Mtuhumiwa aruka kwenye gari la polisi na kukimbia wakati akipelekwa mahakamani


Mtuhumiwa Mohammed Mwalim Ali mkaazi wa Pujini kisiwani Pemba anaekabiliwa na shitaka la wizi na unyang’anyi ametoroka na kukimbia kusikojulikana wakati akipelekwa mahakamani akiwa chini ya uangalizi wa Polisi.
Mtuhumiwa huyo alichupa katika gari ya polisi wakati iliposimama nje ya mahakama ya Mkoa Chake Chake alipofikishwa leo asubuhi kwa ajili ya kwenda kujibu  kesi hiyo inayomkabili.
Mtuhumiwa huyo na wenzake watano wanatuhumiwa kufanya wizi wa fedha riali 250 sawa na milioni mbili za kitanzania pamoja na vito mbali mbali vya mapambo ikiwemo mikufu, pete na vitu vyengine vyenye  thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3, mali ya Moza Hilal Shamis mkaazi Kichaka Mtangani Mkoani Pemba .
Imedaiwa mahakamani hapo Mtuhumiwa Mohammed Mwalim Ali, na wenzake Saleh Juma Muhene , Othaman Awesu Bakar, Khalfan Mwalim Khalfan(Fangasi,  Khamis Juma Hemed, kinyume cha Sheria walitenda kosa la uvamizi na kuiba, huku Bi Mgeni Amour Kombo (32) akituhumiwa kupokea mali za wizi.
Hakim wa Mahakama ya Mkoa Chake Chake Khamis Ali Simai ameagiza kutafutwa na kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kufikishwa mbele ya mahakama hiyo, huku washitakiwa namba 3 na 4 Othman Awesu Bakar na Khalfan Mwalim Khalfan wakirejeshwa rumande hadi April 27 mwaka huu, wengi watatu wamepatiwa dhamana.

0 Responses to “Mtuhumiwa aruka kwenye gari la polisi na kukimbia wakati akipelekwa mahakamani ”

Post a Comment

More to Read