Friday, April 7, 2017

WANANCHI KYELA WAANDAMANA KUPINGA MAUAJI


Shughuli za kiuchumi katika mji mdogo wa Ipinda wilayani Kyela zimesimama kwa zaidi ya saa tano baada ya wananchi na wafanyabiashara wa mji huo kuandamana wakipinga vitendo vya uhalifu hasa mauaji na wizi wa kutumia nguvu ambavyo wanadai kuwa vikekithiri katika siku za hivi karibuni katika mji huo.


Wakazi wa mji mdogo wa Ipinda wilayani Kyela kwa umoja wao wameingia mitaani, wakiandamana kwa lengo la kupaza sauti zao kupinga vitendo vya uhalifu hasa mauaji na wizi unaoendelea kwenye mji huo huku wakilalamikia askari polisi wa kituo chao cha Ipinda kuishi mjini Kyela na kusababisha mji huo kutokuwa na ulinzi wa aina yoyote nyakati za usiku.
Wazee maarufu wa mji wa Ipinda wamesema walijenga kituo cha polisi katika mji huo kwa nia ya kukabiliana na uhalifu,lakini wanashangaa kuona hali imekuwa kinyume na matarajio yao kwani badala ya uhalifu kupungua umeongezeka.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mji wa Ipinda Mang’ati Baton Mwambungu amesema katika kipindi cha muda mfupi wa chini ya mwezi mmoja maduka zaidi ya 20 yamevunjwa,nyumba za makazi takriban nne zimevamiwa na mauaji ya watu kadhaa yametokea.
Akizungumza kwa njia ya simu,Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kyela,Claudia Kitta amesema hajawahi kupata taarifa za matukio ya uhalifu katika mji huo na kwamba maandamano na malalamiko ya wananchi hao ni haramu.

0 Responses to “WANANCHI KYELA WAANDAMANA KUPINGA MAUAJI”

Post a Comment

More to Read