Friday, April 7, 2017
Mke auawa na Mumewe kwa Imani za Kishirikina
Do you like this story?
Mtu mmoja
katika kijiji cha Solwe wilayani Kwimba mkoani Mwanza anashikiliwa na
jeshi la polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe kutokana na imani za
kishirikina.
Tukio hilo limetokea tarehe 5/04/2017 saa 5 asubuhi ambapo mtu huyo
anayefahamika kwa jina la Kumalija Kondolo Basu anadaiwa kumchoma mke
wake na kitu chenye ncha kali sehemu za kichwani na shingoni upande wa
nyuma na kupelekea kifo chake papo hapo.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alikuwa akiishi na mkewe nyumbani kwake kijiji
cha Bagadu wilayani Magu lakini hivi karibuni alikwenda kwa wakwe zake
wilayani Kwimba kuwasalimia yeye pamoja na mkewe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa mwanza DCP Ahmed Msangi amesema kuwa siku ya
tukio mtuhumiwa alibaki nyumbani na mkewe kwani wengine walikuwa
wamekwenda gulioni kwasababu ilikuwa siku ya gulio.
Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, inadaiwa kuwa baada ya mtuhumiwa kuona
wanafamilia hawapo ndipo alimchukua mkewe na kuingia naye ndani na kisha
kutekeleza kitendo hicho.
Amesema wananchi walitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo ambapo
askari walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kufanikiwa
kumakamata mtuhumiwa.
Amesema mtuhumiwa wa mauaji hayo amekamatwa na yupo katika mahojiano na
jeshi la polisi, pindi uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)