Friday, May 5, 2017
Ufafanuzi kuhusu upimaji wa VVU nyumba kwa nyumba
Do you like this story?
Baada ya taarifa kusambaa katika mitandao ya Instagram, ikimnukuu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Grace Magembe akisema kuwa “Upimaji wa VVU nyumba kwa nyumba sasa rasmi, mchakato unaendelea na zoezi litaanza rasmi mwishoni mwa mwezi huu”, ofisi hiyo imetolea ufafanuzi taarifa hizo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mara nyingine, inapenda kutoa ufafanuzi kwamba UKIMWI HAUPIMWI NYUMBA KWA NYUMBA bali inafanya utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania ambapo UKIMWI ni ugonjwa mmojawapo unaopimwa katika utafiti huu. Aidha, utafiti huu unafanyika kwenye kaya chache ambazo zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili ziweze kuwakilisha kaya nyingine ambazo hazihusiki moja kwa moja. Utafiti huu unajumuisha kaya zipatazo 16,000 ambazo ni sampuli iliyochaguliwa kisayansi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na unahusisha watu wazima wasiopungua 40,000 na watoto takribani 8,000.
Kwa Dar es Salaam, utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI utahusisha kaya zisizozidi 1,000
kati ya kaya 1,000,000 na unatarajia na kuanza tarehe 31 Mei, 2017 na kuendelea kwa wiki zisizozidi tatu (3).
Mbali na upimaji wa UKIMWI, utafiti huu pia unapima kiwango cha maambukizi ya Kaswende, Homa ya ini (Hepatitis B), uwepo wa viashiria vya usugu wa dawa, maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha VVU mwilini kwa watu wanaoishi na VVU (Viral load), wastani wa maambukizi ya VVU kwa watu wa rika zote pamoja na wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4 T-cell count). Aidha, kupima ni hiari na watakaogundulika kuwa na maambukizi, watapata rufaa ya kwenda kupatiwa matibabu bure katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Ifahamike kwamba, utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/17 unafanyika nchini kwa mara ya nne (4) ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2003, wa pili mwaka 2007 na wa tatu mwaka 2011. Hivyo, NBS inapenda kuwatoa hofu Wananchi kuwa, kufanyika kwa utafiti huu sio jambo jipya na Watanzania ambao wamekuwa wakipitiwa na utafiti huu, wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya asilimia 90 na mpaka sasa utafiti huu umeshafanyika katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na kwa upande wa Tanzania Zanzibar, utafiti huu umekamilika katika maeneo yote yaliyochaguliwa.
Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania unaendelea kufanyika nchini, ukisimamiwa na NBS kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “Ufafanuzi kuhusu upimaji wa VVU nyumba kwa nyumba”
Post a Comment