Friday, April 4, 2014

JAJI WARIOBA AISHANGAA SERIKALI.




Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema waliokuwa wajumbe wa tume hiyo hawajawahi kudai malipo ya pensheni ya Sh200 milioni kama inavyodaiwa.

“Wajumbe wa Tume hawajatoa madai ya kulipwa shilingi milioni mia mbili. Hakuna mjumbe yeyote aliyetoa dai kama hilo na Serikali inajua,” alisema

Jaji Warioba katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, aliyoitoa kupitia Nyalali, Warioba and Mahalu Law Advocates ali ongeza:

“Nimeona taarifa iliyotolewa na Serikali kuhusu Tume ya Mabadiliko, nimeshangazwa na maudhui na lugha iliyotumika,” alisema Warioba akirejea taarifa iliyotolewa na Ikulu juzi ikieleza jinsi tume hiyo ilivyohitimisha kazi zake.

Wiki hii Jaji Warioba alikaririwa akilalamika jinsi yeye na makamishna wake walivyoondolewa ofisini na kunyang’anywa magari kwa haraka bila kusubiri siku waliyopanga kufanya makabidhiano, lakini Ikulu ilimjibu kwamba shughuli za Tume hiyo zilikoma siku ambayo Tume ilivunjwa.

Katika taarifa yake ya jana, Jaji Warioba alisema aliwasilisha Rasimu ya Katiba Machi 18 mwaka huu na Tume ilivunjwa Machi 19 wakati wajumbe wakiwa bado mjini Dodoma.
“Pamoja na lugha ya kejeli inayotumiwa na Serikali kuniita mnafiki, busara ya kawaida ilitakiwa kutumika kufanya maandalizi ya kuwarudisha wajumbe nyumbani na kuandaa makabidhiano,” alisema.

Alisisitiza kuwa Serikali ilikuwa na wajibu wa kuwarejesha makwao wajumbe wa tume hiyo, hata kama muda wa kisheria wa kufanya kazi ulikuwa umepita.

“Niliwasilisha Rasimu Machi 18, 2014. Tume imevunjwa Machi 19, 2014 wakati wajumbe wako Dodoma. Pamoja na lugha ya kejeli iliyotumiwa na Serikali na kuniita mnafiki, busara ya kawaida ingeonyesha umuhimu wa Serikali kujipa muda wa kufanya maandalizi ya kuwarudisha wajumbe nyumbani,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:

“Hata kama sheria ilitaja muda wa kuvunja Tume bado ilikuwa ni wajibu Serikali kufanya mipango ya safari ya wajumbe baada ya kumaliza kazi. Sheria haikuizuia Serikali kufanya hilo. Huo ni wajibu wa Serikali na utaratibu wa kawaida unaotumiwa na Serikali kwa tume zote inazoziunda. Inaonekana Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliwekewa utaratibu tofauti. Kulikoni?”.

0 Responses to “JAJI WARIOBA AISHANGAA SERIKALI.”

Post a Comment

More to Read