Friday, April 4, 2014
MGOMVI WA MKE WA ZUMA ATISHIA KUJIUA.
Do you like this story?
Dar es Salaam. Akiwa amekaa mahabusu kwa zaidi ya miezi miwili,
Mtanzania Steven Ongolo, anayeshikiliwa kwa kutishia kutoa siri za Nompumulelo
Zuma (ManTuli), ambaye ni mke wa rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ametishia
kujiua akidai anatishiwa kuuawa na haki kutotendeka katika kesi yake.
Ongolo alikamatwa na polisi jijini Durban
Januari mwaka huu baada ya kudai kuwa ana siri nzito zinazomuhusu mke wa Rais
Zuma, huku akitishia kuanika siri hizo.
Mapema wiki hii, Ongolo, ambaye anashikiliwa
katika mahabusu ya Pietemaritzburg, aliomba kuonana na waandishi wa habari na
kuwaambia kuwa atajiua wakati wowote kwa sababu ananyanyasika katika mahabusu
hiyo.
“Nataka kumaliza kila kitu hapa kwa sababu
najua sitapata haki katika kesi hii. Nimeandika barua na kueleza kila kitu,”
alisema Ongolo. Kwa Afrika Kusini, mahabusu anaweza kupata fursa ya kuzungumza
na waandishi wa habari kueleza malalamiko yake.
Pia Ongolo ambaye amenyimwa dhamana kwa mara
ya pili, alieleza anapata shida zaidi kutoka kwa mahabusu wenzake ambao
wanamtukana na kumsimanga, wakidai eti anamsababishia matatizo rais wao.
“Watu humu ndani wananiuliza kwa nini
nasababisha matatizo kwa familia ya rais. Nahofia maisha yangu, chochote
kinaweza kunipata,” alisema.
Hata hivyo, Ongolo licha ya kuahidi
kuwakabidhi waandishi wa habari nakala ya barua yake ya kutaka kujiua, baadaye
alisema barua hiyo imechukuliwa.
Pamoja na malalamiko mengine, Ongolo alisema
anahisi kuna mchezo mchafu unaofanyika kwani hata wakili wake, Lekoko Lekoa
ameacha kufika mahabusu kumsalimia ili kutimiza mipango waliyopanga.
“Nitajitetea peke yangu mahakamani. Katika
nchi za watu najua haki haiwezi kutendeka,” alisema.
Ongolo alikamatwa Januari 24 mwaka huu baada
ya kufanya mahojiano na gazeti la Sunday Tribune. la nchini humo na kueleza
kuwa ana siri nzito zinazomuhusu mke wa Rais Zuma.
Mtanzania huyo alisema, ManNtuli anajua kwa undani
sababu ya kifo cha mlinzi wake, Phinda Thomo, ambaye aliripotiwa kujipiga
risasi bafuni kwake, Soweto mwaka 2009.
Ongolo alituma ujumbe wa baruapepe kwenye
magazeti ya Afrika Kusini akidai kuwa Thomo hakujiua, bali aliuawa kutokana na
siri za mahusiano kati yake na MaNtuli kuvuja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MGOMVI WA MKE WA ZUMA ATISHIA KUJIUA.”
Post a Comment