Tuesday, June 10, 2014

MSICHANA WA KAZI ALIYECHOMWA NA PASI NA KUTESWA NA BOSI WAKE KWA MIAKA 3 AKABIDHIWA KWA WANAHARAKATI






Hatimaye Yusta Lucas (20), binti aliyekuwa akiteswa kwa kuchomwa pasi na kung’atwa na mwajiri wake, Amina Maige ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Mwananyamala alikokuwa amelazwa na kukabidhiwa kwa wanaharakati wa Taasisi ya Jipange.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya maridhiano kati ya Ustawi wa Jamii, mama mzazi wa Yusta, Modesta Simon, Kamati ya Ulinzi na Usalama Kata ya Makumbusho na Jipange ambao ndiyo iliyofanikisha kumwokoa binti huyo.

Akizungumza jana, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makumbusho, Husna Nondo alisema baada ya kutafakari kwa kina juu ya usalama na urahisi wa kupatikana pale atakapohitajika, wamekubaliana binti huyo akae kwa muda kwa mmoja wa wanakikundi kutoka taasisi hiyo.
“Tumeafikiana Yusta aendelee kubaki mikononi mwa wanaharakati ili iwe rahisi kupatikana atakapohitajika mahakamani, maana yeye ndiye shahidi wa kwanza. Mama na mjomba wake waliotoka Tabora wataendelea kukaa Upanga walikofikia,” alisema Nondo.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Mwananyamala, Rose Temu alisema wamemkabidhi Yusta kwa Jipange kwa maandishi na wanaamini yuko katika mikono salama kwa sababu taasisi hiyo ndiyo iliyokuwa mstari wa mbele kumuokoa.

“Wakati akisubiri kesi yake, tumekubaliana awe chini ya Jipange tumeona asiendelee kukaa wodini kwan anaweza kupata ugonjwa mwingine, uamuzi ambao hata mama yake ameuridhia.”

Mwenyekiti wa Jipange, Janet Mawinza alisema wamekubali kumpokea Yusta kwa ajili ya usalama wake lakini akasema hataeleza ni wapi atakuwa anaishi kwa kipindi atakachokuwa akisubiri kesi.

“Sisi tumempokea kama kikundi na tunachoomba ni vyombo vinavyohusika na suala hili kuhakikisha vinashughulikia suala lake kwa wakati ili huyu binti aungane na familia yake Tabora,” alisema.

Mama wa binti huyo alisema anaamini binti yake yuko katika mikono salama. “Hawa Jipange ndiyo walikuwa naye tangu siku ya kwanza na sioni kama kuna tatizo wao kuendelea kuwa naye.”

Kwa siku tano, Yusta alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala kuuguza majeraha yanayodaiwa kusababishwa na kung’atwa na kuchomwa na pasi na Maige ambaye alikuwa mwajiri wake huko Mwananyamala Kwa Manjunju kwa muda wa miaka mitatu.

Mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi katika Kituo cha Oysterbay na wakati wowote atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Credit:  Mwananchi


0 Responses to “MSICHANA WA KAZI ALIYECHOMWA NA PASI NA KUTESWA NA BOSI WAKE KWA MIAKA 3 AKABIDHIWA KWA WANAHARAKATI ”

Post a Comment

More to Read