Thursday, June 5, 2014
MWENGE WA UHURU WAPATA AJALI, POLISI WATATU WAJERUHIWA
Do you like this story?
Askari
polisi watatu kati ya watano, wameumia vibaya baada ya gari walilokuwa
wakisindikizia Mwenge wa Uhuru kupata ajali mkoani Singida huku waandishi wa
habari na wapigapicha wakinyang’anywa vitendea kazi na kiongozi wa Mbio za
Mwenge, Rachel Steven.
Kitendo
hicho kilielezwa kuwa ni kuwazuia waandishi wa habari kutuma taarifa za ajali
hiyo kwenye vyombo vyao vya habari. Mzozo mkali uliibuka kwa waandishi wa
habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kituo cha Televisheni cha ITV
na Redio One na mwandishi wa Redio Standard waliokuwa kwenye msafara huo.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Singida, (SACP), Geofrey Kamwela alipotafutwa ili aelezee tukio,
alisema hana taarifa kamili na kutaka apewe muda ili afutilie suala hilo aeleze
ajali hiyo. Hata hivyo baadaye alipotafutwa jioni alipotafutwa alisema kuwa
atatolea taarifa suala hilo leo.
Ajali hiyo
iliyohusisha magari matatu ilitokea katika Kijiji cha Kirumbi, Wilaya ya
Sikonge, mpakani mwa mikoa ya Tabora na Singida ikiwa ni siku ya kwanza ya mbio
za Mwenge huo ulioingia mkoani Singida ukitokea Mkoa wa Mbeya.
Mashuhuda
wa ajali hiyo, walisema kuwa ilitokea muda mfupi baada ya Mwenge kupokewa
katika Kijiji cha Rungwa kilichopo Kata na Tarafa ya Itigi. Ilielezwa kuwa gari
moja la polisi lililokuwa kwenye msafara lilipasuka gurudumu na kusimama
pembeni mwa barabara.
Gari
jingine la polisi lililokuwa kwenye msafara lilisimama ghafla kutaka kufahamu
kilichowapata wenzao, ndipo gari la Ofisi ya Afya ya Mkoa likiwa na wahudumu wa
afya, lililigonga kwa nyuma gari hilo.
Kwa kuwa
kila gari lilikuwa kwenye mwendo wa kasi ili kuendana na gari la Mwenge
lililokuwa limetangulia, gari jingine lililokuwa na askari waliokuwa
wamening’inia juu nalo lililigonga gari hilo la afya kwa nyuma na kusababisha
askari hao kuumia.
Katika
tukio hilo, hakuna hata mmoja kati ya wahudumu wa afya aliyeumia, lakini ajali
hiyo ilisababisha askari mmoja kuvunjika mguu, mwingine kuvunjika mkono huku
wawili hali zao zikiwa nzuri na mwingine alikuwa mahututi.
Baada ya
tukio hilo, waliwahishwa kwenye Hospitali ya Misheni ya St. Gasper iliyopo
Itigi kwa matibabu zaidi.
>>Mwananchi
>>Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MWENGE WA UHURU WAPATA AJALI, POLISI WATATU WAJERUHIWA ”
Post a Comment