Wednesday, September 10, 2014
IPTL YAMDAI ZITTO KABWE FIDIA YA SHILINGI BILIONI 500
Do you like this story?
Kampuni ya kufua
umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), imefungua kesi ya madai
katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakimtaka Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe awalipe fidia ya Sh bilioni 500 kutokana na kutoa kashfa
dhidi yao.
IPTL, Kampuni ya Pan
Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP) na Mwenyekiti Mtendaji wa
makampuni hayo mawili, Harbinder Seth wamefungua kesi dhidi ya Zitto, Mhariri
wa gazeti la Raia Mwema, Kampuni ya Raia Mwema na Kampuni ya Flint Graphics.
Washitakiwa wengine
wameshitakiwa kwasababu makala yenye maneno ya kashfa na kuwachafua,
iliyochapishwa Agosti 13 mwaka huu katika ukurasa wa 7 na 14 wa gazeti lao,
ikiwa na kichwa cha habari cha "Fedha za IPTL ni Mali ya Umma"
na Kampuni ya Flint Graphics kwa kuchapisha gazeti hilo.
Aidha, wanaiomba
Mahakama iamuru makala hayo, yalikuwa ya upotoshaji na kuwachafua kwa
kudhamiria, pia wadaiwa waombe radhi kwa kuchapisha habari ya kuomba
msamaha kwenye kurasa za mbele katika matoleo mawili mfululizo ya gazeti hilo.
Wadaiwa hao waliiomba
Mahakama, itoe zuio kwa wadaiwa, watumishi wao, wafanyakazi, washirika,
wawakilishi au watu wengine wanaofanya kazi chini ya wadaiwa, kuchapisha
au kuandika makala yoyote ya kuwachafua.
Wanadai makala hayo
yalikuwa na maneno “kwa mara nyingine
Serikali kupitia viongozi wake akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
wamedai kwamba dola milioni 250 za Kimarekani zilizopaswa kuendelea kuwepo
katika akaunti ya “Tegeta Escrow Account’ si mali ya Serikali na hivyo si mali
ya umma…. Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na
Madini, Shirika la Tanesco pamoja na IPTL”.
Ilidaiwa kuwa kabla
ya kusambaza habari hizo, wadaiwa walitakiwa kufanya juhudi za
kuthibitisha ukweli kutoka kwao au kwa maofisa husika wa Serikali, ambao
wangethibitisha ukweli kuwa fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya Escrow,
zilikuwa ni dola milioni 122 za Kimarekani na siyo dola milioni 250, kama
walivyodai.
Aidha, wangejua fedha
ziliwekwa katika makubaliano ya Escrow ;na siyo kama fedha za umma, lakini ni
kutokana na mgogoro wa malipo, yaliyotakiwa kufanywa na Tanesco kwa IPTL.
Wadai hao walifungua
kesi hiyo Septemba 4, mwaka huu kupitia kwa Wakili Melchisedeck Lutema na
Kay Felician Mwesiga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “IPTL YAMDAI ZITTO KABWE FIDIA YA SHILINGI BILIONI 500 ”
Post a Comment