Wednesday, September 10, 2014
UAMUZI MGUMU,RAIS HATAONGEZA MUDA BUNGE LA KATIBA.
Do you like this story?
Dodoma. Makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na
viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kutaka Bunge Maalumu lifikie
ukomo Oktoba 4, mwaka huu yamezua sintofahamu mjini hapa huku uamuzi huo
ukionekana kuwachanganya viongozi wa Bunge hilo.
Kutwa nzima ya
jana, viongozi wa Bunge Maalumu walishinda kwenye vikao vya mashauriano huku
wabunge wa CCM wakitarajiwa kukutana jana usiku kwenye makao makuu ya chama
hicho kupewa taarifa rasmi za uamuzi huo.
Katika
makubaliano baina ya TCD na Rais Kikwete, imeamuliwa kuwa uamuzi wa Rais
kupitia Tangazo la Serikali (GN) 254 la kuongeza siku 60 hadi Oktoba 4
uheshimiwe na baada ya tarehe hiyo Bunge liahirishwe.
Uamuzi huo ni
kinyume cha azimio la Bunge Maalumu la Agosti 5, 2014 ambalo lilirekebisha
Kanuni ya 14 (4) na kuifuta Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi, pia
sikukuu na siku za Jumapili.
Mwenyekiti wa
Bunge, Samuel Sitta alikaririwa akiwaambia wajumbe wa Bunge hilo kwamba Rais
alikuwa ameridhia kwamba siku 60 alizotoa hazingejumuisha Jumamosi, Jumapili na
siku za sikukuu.
Ni kwa msingi
huo, Bunge hilo likapanga kwamba lingeendelea na shughuli zake hadi Oktoba 31,
wakati Mwenyekiti wa Bunge atakapokabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais
Kikwete.
Hata hivyo,
makubaliano yaliyofikiwa baina ya viongozi wa TCD na Rais yanaonekana kuvuruga
kabisa ratiba ya Bunge hilo ambalo jana na juzi, Kamati ya Uongozi ilikutana
mara kadhaa kuona jinsi ya kunusuru mchakato huo.
Ingawa
haikufahamika mara moja kama vikao hivyo vya kamati ya uongozi inayoongozwa na Sitta
mwenyewe vinajadili nini, lakini taarifa zimedai huenda kukawa na mabadiliko
makubwa ya ratiba.
Habari
nyingine zinadai kwamba mabadiliko hayo huenda yakapunguza muda wa baadhi ya
shughuli za kazi za Bunge hilo ili liweze kukamilisha kazi yake ikiwamo wajumbe
kupiga kura ya uamuzi.
Katika kikao
cha jana asubuhi, kamati hiyo ilishindwa kurekebisha ratiba yake ili iendane na
siku zilizosalia, hivyo kuahirishwa kwa kuwapa kazi wataalamu wake kuleta
mapendekezo ambayo yangejadiliwa jana mchana.
Katibu wa Bunge
Maalumu, Yahya Khamis Hamad alithibitisha jana kwamba ratiba ya Bunge
imebadilika kutokana na hoja nyingi kukubalika ndani ya kamati.
“Kamati ya
uongozi itakutana baadaye (jana) kuangalia vipengele ambavyo hawakukubaliana
kwenye kamati ndivyo wavipangie muda na ratiba itajulikana baada ya kikao
hicho,” alisema Hamad.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “UAMUZI MGUMU,RAIS HATAONGEZA MUDA BUNGE LA KATIBA.”
Post a Comment