Wednesday, October 8, 2014
FFU NJOMBE WATUMIA MAMBOMU YA MACHOZI KUTULIZA VURUGU ZA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI NJOSS ,WANAFUNZI WACHOMA MOTO BWENI
Do you like this story?
| Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Njombe, Fulgence Ngonyani akiangalia bweni la wanafunzi wa shule ya sekondari Njombe ambalo limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo. |
| Askari akimwangalia mmoja wa wanafunzi ambaye anapelekwa kupakizwa kwenye gari kwa ajili ya kwenda kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi. |
| Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Njombe, Fulgence Ngonyani akitazama gari dogo ambalo ni la mwalimu Benard Nyamahonga lililovunjwavunjwa vioo vyake na wanafunzi hao. |
Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Njombe
wakiwa wamewaweka chini ya ulinzi baadhi ya wanafunzi wa shule ya
sekondari Njombe (Njosi) wakati wakisubiri kupelekwa kituo cha polisi
leo.
|
ASKARI
wa kutuliza ghasia (FFU) mkoa wa Njombe leo walazimika
kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi wa shule ya
sekondari Njombe (NJOSS )baada ya vurugu kubwa kuibuka jana katika
shuleni hapo kwa wananfunzi wa shule hiyo ya wavulana
kuteketeza kwa moto bweni la shule hiyo pamoja na
kuharibu majengo ya shule ya Msingi Kilimani kwa mawe .
Kutokana na
vurugu hizo shule hiyo imefungwa kwa muda wa
mwezi mmoja kuanzia sasa ili kupisha ukarabati mkubwa wa
majengo ya shule hiyo .
Afisa Elimu wa Mkoa wa Njombe, Said Nyasiro alitoa agizo la
kufungwa kwa shule hiyo kwa mwezi huo mmoja hadi
Novemba 8 huku wanafunzi hao wakitakiwa kurejea shuleni hapo na
kiasi cha shilingi 150,000 kila mmoja kama fidia ya mali zilizoharibiwa
Katika tukio hilo, askari polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi
kuwatawanya wanafunzi waliokuwa wakifanya vurugu, wanaosoma Kidato cha Tano na
Sita, ambao walifanya uharibifu wa kuchoma moto eneo la shule linalozunguka
lenye miti na kuharibu pia gari dogo Toyota Carina namba: T809 BBX la Mwalimu
wa Nidhamu, Benard Nyamahonga kwa kulivunjavunja vioo kwa mawe.
Kama hiyo haitoshi, wanafunzi hao walikwenda katika nyumba ya mwalimu
mkuu wa shule hiyo, Benard William na kurusha mawe yaliyovunja vioo vya
madirisha ya nyumba hiyo.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgence
Ngonyani pamoja na maofisa wa Upelelezi kutoka jeshi hilo alithibitisha kutokea
tukio hilo na kufanya ukaguzi wa kutembelea maeneo yaliyoharibiwa, sambamba na
kupata taarifa za awali kutoka kwa walimu wa shule hiyo.
Kamanda Ngonyani ambaye alikataa kuzungumzia kwa undani juu ya tukio
hilo, ambapo alisema bado wanachukua maelezo, alisema taarifa rasmi ya juu ya
upelelezi wa tukio hilo itatolewa.
Hata hivyo askari wa Jeshi la Polisi, walikuwa wamezunguka katika eneo
lote la shule ya Sekondari Njombe kwa ajili ya kuweka ulinzi kuhakikisha hakuna
wanafunzi yeyote anayetoroka kwa ajili ya hofu ya kukamatwa.
Askari hao ambao walikuwa wamevaa dhana zao za kudhibiti fujo wakiwemo
askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) pamoja na askari wa upelelezi,
katika hatua ya awali ya kuwabaini wanafunzi waliofanya uharibifu huo,
waliitisha paredi ya wanafunzi wote na kufanya uhakiki wa kubaini waliohusika
na tukio hilo.
Katika zoezi hilo la utambuzi, zaidi ya wanafunzi zaidi ya 40 walitambulika
awali kuwa vinara wa vurugu hizo, ambapo walipandishwa kwenye magari mawili ya
polisi kupelekwa kituo kikuu cha polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo lilivyotokea, Isabela Malangalila, Ofisa
Mtendaji wa Mtaa wa Mpechi na Joshoni ambako ndiko shule hiyo ilipo, alisema
vurugu za wanafunzi kuanza kuchoma moto mabweni hayo zilianza mnamo saa 5 usiku
jana.
“Kabla ya tukio hilo, jana kulikuwa na kikao cha Wazazi na Walimu wa
shule ya sekondari Mpechi ambacho kilikuwa kinawahoji wanafunzi 29 waliokuwa
wamekwenda kwenye disko katika chuo cha Maendeleo ya Jamii bila ya kupata
ruhusa,” alisema Malangalila.
Alisema katika kikao hicho, wanafunzi waliobainika kwenda kwenye disko
hilo akiwemo pia mwanafunzi mmoja aliyekutwa na simu ya mkononi waliambiwa
waandike maelezo, lakini jambo la kushanga baadaye jana usiku wanafunzi zaidi
ya 1000 wanaosoma shule hiyo waliandamana na kuanzisha vurugu huku wakirusha
mawe hovyo na kutishia kuchoma moto shule hiyo.
“Kufuatia vitisho hivyo niliwasiliana na kikosi cha zima moto kufika
haraka kwenye eneo la shule, na hapo ndipo moto ulipoanza kuwaka kwenye bweni
namba nane, baadhi ya wanafunzi walijitahidi kuzima moto uliokuwa ukiwaka
katika bweni hilo,” alisema Malangalila.
Mtendaji huyo wa Mtaa alisema pia, wanafunzi hao waliendelea kufanya
uharibifu zaidi kwa kuvunja duka la shule, kung’oa mboga zilizopandwa kwenye
bustani, kisha kuwasha moto eneo la shule na kwenda kuharibu gari dogo la
mwalimu wa nidhamu ambalo walilivunjavunja kwa mawe vioo vyake pamoja nakuvunja
vioo vya nyumba ya mwalimu huyo.
“Hali hii inatisha na kusikitisha, wanafunzi hao walipofanya huo
uharibifu walikwenda pia katika shule ya Msingi Kilimani na kuvunja madarasa
pamoja na kuchanachana madaftari ya wanafunzi wa shule hiyo ambao wako darasa
la pili, huku wakiwa wameandika maandishi ukutani yakisema ‘Sisi wanafunzi wa
Njosi tumekuja kulala tu’,” alisema Malangalila.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Benard William akizungumzia tukio hilo,
alisema bweni ambalo limeathirika sana kwenye tukio hilo ni lile la namba nane
ambalo linauwezo wa kuchukua wanafunzi 102.
Aidha mwalimu William alisema kwamba chanzo cha wanafunzi hao kufanya
vurugu hizo zinatokana na madai yao kwamba wamechoshwa kunyanyaswa ikiwemo
kuonewa kwa wanafunzi wenzao 30 ambao walisimamishwa masomo.
“Huu ni utukutu usiositahili kuvumiliwa, unakatisha tamaa sana kwetu sisi
walimu, madai yao ambayo wanayalalamikia kimsingi hayajitoshelezi, kwani
walipotoroka kwenda kucheza disko katika chuo cha maendeleo ya jamii mmoja wao
alivunjika mguu na hadi sasa anatembelea magongo,” alisema William.
Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, Maria Mdee akizungumzia tukio hilo
alisema haamini kilichofanywa na wanafunzi hao, na kuliita tukio hilo kuwa ni miongoni
mwa matukio mabaya yaliyogusa sana maisha yake.
“Inasikitisha sana hasa ikizingatiwa kwamba wanafunzi ambao walikuwa
wakiwahoji jana walikuwa bado hawajafukuzwa shule, bali wasimamishwa tu masomo
mpaka hapo watakapo waleta wazazi wao, na Oktoba 7 tulikutana na wazazi na
wanafunzi hao kwa ajili ya kuwaeleza makosa yao,” alisema Mdete.
Alisema kufuatia tukio hilo zima, athari itakuwa kubwa hivi sasa katika
shule hiyo kwa baadhi ya wanafunzi ambao hawakuhusika na tukio hilo, kwani
mwezi Novemba walikuwa wanatarajia kufanya mtihani wa mkoa kabla ya kufanya
mtihani wa Taifa.
Mwenyekiti huyo alisema kufuatia tukio hilo, uongozi wa shule hiyo
utasubili tamko la Afisa Elimu wa mkoa wa Njombe kama shule hiyo itafungwa ili
wanafunzi warejee majumbani hadi hapo baadaye.
Afisa Elimu wa mkoa wa Nkombe, Said Nyasiro akiwa na Ofisa Elimu wa shule
za Sekondari mkoani hapa, Venance Msungu walifika katika eneo la shule hiyo na
kutembelea kuangaria uharibifu uliotokea na kufanya mkutano wa ndani na walimu
wa shule hiyo ambao ulichukua zaidi ya saa mbili, ambapo waandishi wa habari
hawakuruhusiwa kuingia.
Kamanda wa Polisi, Ngonyani akiwa na maofisa wake, pamoja na walimu na
viongozi hao wa wizara ya Elimu walifanya mkutano wa ndani, lakini alipotoka
kwenye mkutano huo aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo
atalizungumzia mara baada ya kufanya tathimini ili kubaini thamani ya mali
zilizotekea.
Hili ni tukio la pili sasa kutokea kwa shule hiyo ya sekondari
Njombe, ambapo mwaka mmoja uliopita, wanafunzi wa shule hiyo walichoma moto
bweni ambalo hivi sasa lipo kwenye ujenzi.
*Mwandishiwetu Michael Katona matukiodaima.co.tz Njombe*
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)

0 Responses to “ FFU NJOMBE WATUMIA MAMBOMU YA MACHOZI KUTULIZA VURUGU ZA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI NJOSS ,WANAFUNZI WACHOMA MOTO BWENI”
Post a Comment