Monday, December 22, 2014

NDIO BASI TENA KWA WACHEZAJI HAWA WA SIMBA NA YANGA




Dar es Salaam. Klabu za Simba na Yanga zimefanya mabadiliko
kwenye vikosi vyao na moja kwa moja watakuwa wameathiri nafasi za baadhi ya
wachezaji wa vikosi hivyo.

Timu zote hizo kongwe zimefanya mabadiliko zaidi katika
kujiimarisha lakini pamoja na mapendekezo mapya yaliyowekwa, imewaweka pabaya
baadhi ya wachezaji na hivyo kufanya wakati wao kuwa mgumu.

Yanga imewasajili Mliberia Kpah Sherman, Mrundi Amissi
Tambwe na Danny Mrwanda kwenye safu ya ushambuliaji na kipa Athumani Majogo,
wakati Simba imewasajili Dan na Simon Sserunkuma, Juku Musheed (wote raia wa
Uganda) na Hassan Kessy. Wafuatao watakalia kuti kavu Simba kipindi hiki;

William Lucian ‘Gallas’

Usajili wa Hassan Kessy aliyetokea Mtibwa Sugar utampa
wakati mgumu beki huyu na kwamba anaweza kuwa chaguo la pili kama si la tatu.
Licha ya kuwa na uzoefu na umri wake bado ukiwa mdogo, Lucian atakuwa na wakati
mgumu wa kupata nafasi mbele ya Kessy, ambaye amekuwa akiwindwa na Simba kwa
kipindi kirefu bila mafanikio hapo awali.


Nassor Masoud ‘Chollo’

Beki huyu mkongwe wa Simba ameonekana kurudisha makali yake
hivi karibuni, lakini inasadikiwa uwepo Kessy utamrudisha tena benchi.

Chollo hajawa na kipindi kizuri kwa takribani mwaka sasa
kutokana na matatizo ya majeraha. Chollo uenda akawa mbadala wa Kessy kwenye
kikosi cha kwanza cha Simba.

Hassan Isihaka:

Hakika amekuwa akifanya kazi kubwa na hata kuaminika kuanza
kwenye michezo yote ya kirafiki na ya ligi kwa msimu huu. Isihaka amekuwa
akicheza sambamba na Joseph Owino lakini hali ilivyo sasa baada ya usajili wa
beki Juku Musheed, huenda akapoteza nafasi.

Shaban Kisiga ‘Marlone’
Licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuichezesha timu na kufunga
mipira ya faulo. Kiungo huyo mshambuliaji anaweza kupoteza nafasi kwa
washambuliaji Dani Sserunkuma na Elius Maguli ambao ni chaguo la kwanza la
Kocha wa Simba Patrick Phiri aliyetokea kwenye klabu ya Gor Mahia ya Kenya.

Said Ndemla

Kiungo huyu amekuwa akijitahidi na mara kadhaa amekuwa
akipata nafasi lakini ujio wa Simon Sserunkuma aliyetokea Express ya Uganda
unaweza kuzima ndoto zake za kungaa kwani anaweza kuishia benchi kwa kusubiri
mchezaji huyo apate nafasi.


Kwa Upande wa Yanga, Mambo yamebadilika na kwamba Kocha mpya
wa klabu hiyo, Mholanzi Hans Van Pluijm na msaidizi wake, Boniface Mkwasa
wanaweza kubadilisha mambo mengi huku wakiwapa wakati mgumu baadhi ya
wachezaji;


Juma Kaseja:

Kipa huyu mkongwe hajaweza kuwa na wakati mzuri kwa kipindi
kirefu tangu asajiliwe Yanga akiwa kama mchezaji huru. Kaseja ameshindwa
kutamba mbele ya Deo Munishi ‘Dida’, ambaye ameshikilia nafasi yake.

Kaseja pia yuko kwenye hatari ya kupotea zaidi kwani
ameshindwa hata kujiunga na timu kipindi hiki ligi iliposimama kwa madai kuwa
anaidai Yanga lakini pia Yanga hawaheshimu mkataba wake.

Danny Mrwanda:

Pengine usajili wake Yanga umeikomoa Simba lakini Mrwanda
ana wakati mgumu wa kupata nafasi mbele ya mshambuliaji Amissi Tambwe na Kpah
Sherman. Mrwanda ni mchezaji mzoefu na mwenye uwezo wa juu, lakini atakuwa na
wakati mgumu kwenye utafutaji wa namba kikosi cha kwanza Yanga.


Jerryson Tegete:

Tegete bila shaka amechemka, licha ya kuibuka mara kwa mara
na kisha kutoweka tena, yupo kwenye nafasi ngumu hasa kutokana na ujio wa
Tambwe, Mrwanda na Sherman.


Andrey Coutinho:

Baada ya Maximo kutupiwa virago, kiungo Andrey Coutinho
huenda akajikuta kwenye wakati mgumu kutokana na falsafa za Hans Van Pluijim,
ambaye tayari alikuwa ametengeneza wachezaji wake kabla ya kuachana na Yanga
Mei mwaka huu.

Hussein Javu:

Mshambuliaji huyu anaweza kukumbana na changamoto kama
anazozipata mwenzake Tegete. Atahitajika aweke juhudi za hali ya juu kwa kuwa
ndiyo kwanza ametokea majeruhi pia hajaweza kupata muda mwingi wa kucheza.

0 Responses to “NDIO BASI TENA KWA WACHEZAJI HAWA WA SIMBA NA YANGA”

Post a Comment

More to Read