Monday, December 22, 2014

TWIGA CEMENT YAZINDUA CHAMA CHA MAKIPA TANZANIA. TASWA FC WAFUNGUA NJIA.




Kampuni ya Twiga Cement ya jijini Dar es Salaam, jana imefanikiwa kuzindua rasmi Chama cha Wachezaji wa Nafasi ya Golikipa wanaoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania, ambapo katika uzinduzi huo timu hiyo ya Makipa ilicheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya Timu ya Kombaini ya Waandishi wa Habari TASWA F.C.uliofanyika kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama jijini Dar es Salaam jana.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa na Ushindani wa Kipekee kutokana na Timu zote kuwa na Wachezaji Nyota na Tegemeo katika Vipaji vyao, Mashabiki waliofika kushuhudia mchezo huo walifurahishwa na jinsi kila mchezaji alivyoonyesha Ujuzi binafsi na kiwango cha hali ya juu. Timu ya makipa ndiyo iliyokuwa ya kwanza kufanya shambulizi kwenye lango la timu ya TASWA ambapo dakika ya 26 mchezaji Shaaban Kado alikosa Penalt kutokana na beki wa Taswa Martin Peter kunawa akiwa eneo la kumi na nane na penalt hiyo ilidakwa na kipa nyota wa TASWA Ahmed Famau.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika kikosi cha timu ya Makipa kilikuwa mbele kwa bao 1-0,lililofungwa na Juma Kaseja baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa TASWA, ambapo kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko ambapo Taswa iliwatoa, Majuto Omary, Ibrahim Masoud, Ally Mkongwe, Zahoro Mlanzi, Shafii Dauda, na nafasi zao kuchukuliwa na Salum Jaba, Juma Ramadhani, Hatibu Naheka,na Paul Limoy,mabadiliko ambayo hata hivyo yalishindwa kupunguza kasi ya wachezaji hao Makipa wa Ligi kuu waliokuwa muda wote wakilisakama lango la TASWA FC.

Pamoja na kuwa na wachezaji wa akiba timu ya Makipa lakini walishindwa kufanya mabadiliko, kutokana na wachezaji wengi kuwa na pumzi ya kuwamudu TASWA ambapo Makipa hao walisaidiwa na mlinda mlango kutoka timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars, Fatuma Omary ambaye hata hivyo alionyesha kiwango kikubwa baada ya kudaka michomo ya wazi kutoka kwa washambuliaji wa Taswa,Ibrahim Masoud, Shafii Dauda,Majuto Omary pamoja na Ally Mkongwe waliokuwa wakilisakama Lango la timu ya makipa kila wakati.

goli la pili lilipatikana kunako dakika ya 67 kupitia kwa Ivo Mapunda aliyefunga kwa shuti kali lililomshinda mlinda wa TASWA Ahmed Famau,kabla ya shaaban Kado kuhitimisha Kapu la Magoli kwa timu hiyo ya Makipa.

0 Responses to “TWIGA CEMENT YAZINDUA CHAMA CHA MAKIPA TANZANIA. TASWA FC WAFUNGUA NJIA. ”

Post a Comment

More to Read