Saturday, June 20, 2015

MUFTI MPYA KUPATIKANA NDANI YA SIKU SABA.




Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata),  limesema litatangaza mrithi wa Mufti wa Tanzania ndani ya siku saba kuanzia jana.

Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila, alisema utaratibu unaendelea kuhakikisha katika kipindi hicho jina la Mufti mpya linapatikana.

Kuchaguliwa kwa kiongozi huyo mpya wa waumini wa dini ya Kiislam nchini, kunafuatia kufariki kwa aliyekuwa Sheikh mkuu, Mufti Issa Shabani Bin Simba usiku wa kuamkia Juni 15 katika Hospitali ya TMJ ya jijini Dare s Salaam.

Mufti Simba alizikwa siku ya pili yake katika makaburi ya Nguzo nane mjini Shinyanga, ambapo mazishi yake yaliongozwa na Rais Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, kidini na vyama vya siasa.

“Mchakato wa kumpata Sheikh Mkuu wetu utakamilika ndani ya siku saba kuanzia sasa, wananchi na waumini wa dini ya kiislam wawe wavumilivu katika kipindi hiki,” alisema Sheikh Lolila.

Katibu mkuu huyo hakutaka kuweka wazi sehemu wanapokutana wajumbe wa Baraza la Ulamaa ambao ndilo lenye mamlaka ya kumchagua kiongozi.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaotajwa kushika nafasi hiyo ni Kadhi Mkuu, Sheikh Abdallah Mnyasi na manaibu wake Sheikh Abubakar Zuber na Sheikh Ali Muhidin Mkoyogile.

Wengine ni Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Salum Ferej, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya, Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa na Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Masoud Jongo.

CHANZO: NIPASHE

0 Responses to “MUFTI MPYA KUPATIKANA NDANI YA SIKU SABA.”

Post a Comment

More to Read