Monday, October 26, 2015
MABOMU YA MACHOZI YARINDIMA MWANZA
Do you like this story?
Polisi mkoani Mwanza wametumia mabomu
ya machozi mapema leo kutawanya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa Chadema
walioingia mitaani kushangilia wakiamini wagombea wao wanaongoza katika matokeo
ya awali.
Tukio hilo limetokea kwenye kituo cha
kupigia kura cha Shule ya Msingi Mlimani, eneo la Butimba, Ghana na Shule ya
Msingi Buzuluga kwenye majimbo ya Nyamagana na Ilemela.
Taarifa toka jijini humo zinasema kundi
la watu waliokuwa vituoni wakisubiri kubandikwa kwa matokeo hayo, lililipuka
kwa shangwe, nderemo na shamrashamra baada ya matokeo hayo kubandikwa na
wasimamizi wa uchaguzi wakiamini wagombea wao wanaongoza.
Mwandishi wetu aliyeko jijini Mwanza
amesema polisi waliingilia kati na kufyatua mabomu ya machozi kutawanya wafuasi
hao.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, mgombea
ubunge wa Chadema na mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo la Nyamagana,
Ezekiel Wenje anachuana vikali na aliyekuwa Meya wa jiji la Mwanza, Stanslaus
Mabula wa CCM.
Katika jimbo la Ilemela, mbunge
anayemaliza muda wake, Highness Kiwia wa Chadema anatetea nafasi yake kwa
kupambana na mgombea wa CCM, Anjela Mabula.
Uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani
umefanyika jana Oktoba 25, mwaka huu ambapo takribani Watanzania milioni 22.7
wamejiandikisha kwenye daftari la kudumu kwa upande wa Tanzania Bara huku kwa
upande wa Zanzibar zaidi ya wapigakura laki tano wamejiandikisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MABOMU YA MACHOZI YARINDIMA MWANZA”
Post a Comment