Friday, December 11, 2015

VITA YA WATU 6 KATIKA NAFASI MBILI, ITAREJESHA MAKALI YA SIMBA SC KATIKA MASHAMBULIZI?




Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Katika mpangilio wa ‘kufikirika’ Simba SC imefanya usajili ambao unakidhi viwango na mahitaji ambayo yalikuwa na mapungufu katika timu yao, lakini suala la kuamini moja kwa moja kwamba usajili wa Daniel Lyanga, Paul Kiongera na Brian Majwega utazaa matarajio pia si la kuwekea asimilia 100 kwa maana tayari timu hiyo imejijengea mazoea ya kufanya usajili kila wakati bila mafanikio.

Magoli 15 katika michezo 9 ya ligi kuu si haba, lakini safu ya mashambulizi awali ilikuwa ikihitaji nyongeza ya wachezaji. Lyanga, namtazama kama straika kiongozi ambaye atawakumbusha Simba baadhi ya vitu ambavyo walivipata kwa muda mfupi kutoka kwa Mbwana Samatta. Huyu ni kijana ambaye anaweza kujitengenezea nafasi na kufunga magoli.

Lyanga ni mmaliziaji wa uhakika ambaye naweza kusema Simba itapata faida kubwa kuwa naye. Kiongera ni kiungo/namba 10, anaweza kucheza vizuri katika safu ya washambuaji wawili. Nadhani ujio wake utakuwa na maana ya ku-boost safu ya mashambulizi na ile ya kiungo katika utengenezaji wa nafasi za magoli. Pia Mkenya huyu ni mchezaji mwenye nguvu, uwezo wa kumiliki mpira kwa kiwango cha juu.

Usajili wa Majwega, huu unaweza kuwa mzuri zaidi endapo Mganda huyo atafikia kiwango kile ambacho kiliwavutia wafuatiliaji wengi wa michuano ya Kagame Cup ambayo ilifanyika Kigali, Rwanda, Agosti mwaka jana. Akiwa KCCA, Magwega alikuwa mfungaji mzuri sana akicheza safu ya mashambulizi ya Brian Omony.

Ni wing-mshambulizi hatari sana, hasa akitokea pembeni ya uwanja, iwe upande wa kulia au ule wa kushoto. Simba inahitaji pia kasi katika wing- zake. Sehemu hizo hazina wachezaji asilia ndiyo maana wachezaji wa nafasi ya kiungo wa kati kama Awadh Juma, Mwinyi Kazimoto, Peter Mwalyanzi wamekuwa wakitumika zaidi kulingana na mifumo ya uchezaji ya kocha, Dylan Kerr. Majwega ana kasi, uwezo wa kupunguza walinzi wa timu pinzani, kufunga na kutengeneza magoli.

Wataongeza ushindani/Ubora na Vita ya namba dhidi ya Kiiza, Mgosi, Ajib



Kerr atakuwa na wachezaji sita wa uhakika katika safu yake ya mashambulizi. Hamis Kiiza ndiye kinara wa magoli katika timu akiwa amekwisha funga jumla ya magoli 8 msimu huu. 

Mganda huyo amekuwa mmaliziaji mkali na tayari ana ‘Hat-Trick’ moja katika ligi msimu huu. Wakati alipokuwa nje ya uwanja katika mechi kama tatu hivi kutokana na majeraha, Simba ilianza ‘ku-safa’ katika ufungaji lakini haitakuwa hivyo tena.

Kiiza atapata ushindani mkubwa wa kuwania nafasi katika timu ya kwanza mbele ya Lyanga na iwapo mshambuaji huyo wa Tanzania atapangwa mara moja tu anaweza kuchukua nafasi kwa kuwa ni mtu mwenye-shabaha kubwa ya kufunga magoli. Ningependa kuona wawili hawa (Kiiza na Lyanga) wakipangwa sambamba na kuongoza safu ya mashambulizi katika mechi dhidi ya Azam FC ikiwa watakuwa ‘fit’.

Nahodha wa timu, Musa Hassan Mgosi hajafunga hata goli moja tangu aliporejea katika timu hiyo msimu huu akitokea Mtibwa Sugar. Mgosi alikuwa mara nyingi akicheza kama ‘pacha’ wa Kiiza na ushirikano wao ulikuwa mzuri tu lakini kazi ya straika ni kufunga magoli. Jukumu ambalo Musa ameshindwa kulifanya. Atakuwa na wakati mgumu zaidi kuingia kikosi cha kwanza kama atashindwa kuipata funguo yake ya magoli.

Kiongera akiwa ‘fit’ atamuweka benchi Mgosi lakini si kazi rahisi ikiwa mshambulizi huyo wa zamani wa Taifa Stars atajirekebisha na kuzitumia vizuri nafasi nyingi ambazo amekuwa akipoteza. Lyanga, Kiongera watapamba kuingia kikosi cha kwanza mbele ya Kiiza na Mgosi huku nyuma yao akiwepo kijana Ibrahim Ajib ambaye tayari amefunga magoli matatu msimu huu.

Simba ndiyo klabu pekee msimu huu katika ligi kuu wachezaji wake kufunga ‘Ha-trick’. Kiiza alifunga wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar na Ajib alifanya hivyo katika gemu dhidi ya Majimaji FC. Majwega anaweza kuingia katika vita hii ya ‘watu 6’ nafasi mbili kutokana na uchezaji wake wa kupenda kufunga magoli ila anaweza kuingia moja kwa moja katika nafasi ya kiungo wa pembeni ambayo kwa sasa ipo wazi.

0 Responses to “VITA YA WATU 6 KATIKA NAFASI MBILI, ITAREJESHA MAKALI YA SIMBA SC KATIKA MASHAMBULIZI? ”

Post a Comment

More to Read