Thursday, January 14, 2016
BARUA YA MAALIM SEIF KWENDA KWA PAPA FRANCIS
Do you like this story?
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad,
amemwangukia Papa Francis kwa kumwandikia barua, akimuomba kutumia ushawishi
wake na Tanzania kumaliza mzozo wa kisiasa kisiwani humo kabla hali haijawa
mbaya.
Kwa mujibu wa barua yake ya Novemba 25, mwaka jana, Maalim
Seif alimwomba Papa kutumia ushawishi alionao kwa serikali ya Tanzania ili
kuhakikisha haki inatendeka na kuepusha vurugu zinazoweza kutokea.
“Ni wiki tatu sasa tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu na hali
hii imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za kuichumi kutokana na
wananchi wengi kuwa na hofu kuhusu mustakabali wa hali hii….watu wanashindwa
kujua nini kitatokea maana wana hofu kwamba hali hii inaweza kuharibu umoja wa
kitaifa kwa watu kuishi kwa upendo bila kujali dini wala kabila,” ilisema barua hiyo.
Barua hiyo ya Maalim Seif ilisema, Zanzibar ina mchanganyiko
wa Waislamu na Wakristo, hivyo hakuna mgawanyiko kwa misingi ya udini lakini
hatua ya wananchi kukosa haki yao ya kidemokrasia kupitia sanduku la kura baada
ya miaka 20 ya chaguzi visiwani humo kunaweza kusababisha vijana ambao
hawafurahishwi na mwenendo huo kutumia njia mbaya kutafuta haki yao.
“Badala ya kuchukua hatua za pamoja kuzuia uovu huu,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo chama chake kilishinda
kwenye uchaguzi mkuu uliopita, imekuwa ikisaidia serikali ya Zanzibar kwa
kutumia askari na majeshi yake kutishia watu wa upinzani,”ilisema.
“Wakati mmishenari wa kikristu alipomuomba Sultan wa
Zanzibar mwaka 1840 kibali cha kujenga asasi ya
kusaidia jamii kwenye eneo lake, Sultani yule ambaye alikuwa Muislamu
alimtambua kama mtumishi wa Mungu aliyekuwa na lengo la kuendeleza neno la
Mungu” ilisema sehemu ya barua hiyo
kwenda kwa Papa.
Iliongeza kuwa, Zanzibar ilipopata Uhuru wake mwaka
1963, kwa kiwango kikubwa watu wake waliishi kwa amani na ushirikiano baina ya
watu wa madhehebu yote ya Katoliki, Anglikana, Sunni, Shia na Hindu na
hakukuwahi kuwa na mgogoro wala hofu ya watu hao kuhitilafiana kwa misingi ya
tofauti ya dini.
Ilisema Chama cha Wananchi CUF kimekuwa kikishinda chaguzi
zote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, lakini haijawahi
kupewa ushindi wake hata muhula mmoja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ BARUA YA MAALIM SEIF KWENDA KWA PAPA FRANCIS”
Post a Comment