Thursday, January 28, 2016
CUF KUTOA TAMKO KUHUSU KURUDIWA UCHAGUZI ZANZIBAR
Do you like this story?
Baraza Kuu la
Chama Cha Wananchi (CUF), leo linatarajia kutangaza uamuzi mzito kutokana na
kikao cha Kamati ya Utendaji, kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam chini ya
Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kikao hicho cha
Kamati ya Utendaji kilifanyika kwa saa tatu kujadili suala la tarehe
iliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya kurudia uchaguzi wa
Zanzibar, uliofutwa Oktoba 28, mwaka jana.
Kamati hiyo
ambayo ilikuwa na ajenda moja pekee, ilijadili na kutoa uamuzi mzito
ambayo yatawasilishwa kwenye Baraza Kuu leo na kutolewa kwa umma.
Mmoja wa
wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ambaye hakutaka kutajwa jina , alisema kuwa
maazimio yaliyotolewa na kikao hicho kilichoanza saa nne asubuhi, yataishangaza
dunia.
Alisema
uchaguzi uliotangazwa na ZEC kuwa utafanyika Machi 20, mwaka huu, ni
batili kwa kuwa tayari mshindi wa uchaguzi huo anafahamika ni Maalim
Seif.
“Jukumu
kubwa la kikao cha Kamati Tendaji kwa mujibu wa Katiba (ya CUF) ni kuandaa
ajenda kwa ajili ya kikao cha Baraza Kuu litakaloanza kesho (leo) na baada ya
hapo tutatangaza msimamo wetu juu ya uchaguzi huo,” kilieleza chanzo hicho.
Kwa mujibu wa
Ofisa Habari wa CUF, Silas Bwire, Kamati ya Utendaji ilikuwa na wajumbe 18
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambao ni viongozi waandamizi wa chama.
Baraza kuu
ambalo linatarajia kufanya kikao chake leo, litakalopokea ajenda zilizojadiliwa
jana, lina wajumbe 60.
Kikao cha
Baraza ambacho kitaongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Twaha Tasilima, kitajadili
kwa kina ajenda zitakazowasilishwa pamoja na kuzitolea uamuzi.
Wakati
hatima ya CUF kushiriki au kutoshiriki uchaguzi wa marudio inatarajia
kufahamika leo, mgawanyiko mkubwa umeibuka miongoni mwa wajumbe wake wa Baraza
Kuu la Uongozi Taifa.
Katika
mgawanyiko huo, wamo wanaopinga kushiriki huku wengine wakitaka chama kuangalia
upya msimamo wa kususia uchaguzi huo.
Akizungumzia
mgawanyiko huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa
Ladhu, alisema kutokana na ukubwa na uzito wa mgogoro wa uchaguzi, mgawanyiko
ni jambo ambalo halikwepeki kwa chama kikubwa kama hicho.
Alisema uongozi
wa chama uko makini katika kujadili ajenda ya mgogoro wa uchaguzi na kuwataka
viongozi na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa na moyo wa subira
wakati Baraza Kuu la Uongozi la Chama linajiandaa kutoa kauli ya mwisho juu ya
hatima ya uchaguzi huo.
Jussa alisema
uamuzi utakaotolewa na Baraza Kuu ndio utakuwa mwongozo kwa wagombea wote wa
chama pamoja na wanachama na watu wanaokiunga mkono chama.
Alisema mchezo
aliyoufanya Jecha wa kufuta matokeo ya uchaguzi kwa manufaa ya CCM, haukubaliki
katika misingi ya demokrasia na utawala bora.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ CUF KUTOA TAMKO KUHUSU KURUDIWA UCHAGUZI ZANZIBAR”
Post a Comment