Monday, February 29, 2016
TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU UGONJWA WA KIPINDUPINDU.
Do you like this story?
Naibu Waiziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,Wazee na Watoto,Dk.Hamis Kigwangala akitoa ufafanuzi kwa wanahabari (hawapo pichani). |
TAMKO
KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. DKT.
HAMISI A. KIGWANGWALLA (MB); NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO, TAREHE 29 FEBRUARI 2016
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Taarifa
hii ni mwendelezo wa utaratibu ambao Wizara yangu imejiwekea kila wiki wa kutoa
taarifa kwa umma kuhusu hali ya kipindupindu nchini pamoja na kueleza juhudi
mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa ili kukabiliana na hali hii. Hadi kufikia
tarehe 28 Februari 2016, jumla ya wagonjwa 16,825 wametolewa
taarifa, na kati ya hao watu 258 wamepoteza maisha.
Takwimu
za wiki iliyopita zinaonyesha kuwa kuanzia tarehe 22 hadi 28 Februari 2016,
idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa ni 473, na kati yao watu 9
walipoteza maisha yao. Takwimu hizi za idadi ya wagonjwa katika wiki hii,
zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa imepungua japo kwa kiasi kidogo sana (5%)
ukilinganisha na wiki iliyopita ambapo wagonjwa 499 waliripotiwa. Katika
wiki iliyoishia tarehe 21 Februari, Mkoa wa Iringa ndio uliokuwa ukiongoza kwa
kuwa na wagonjwa wengi zaidi. Kwa wiki hii idadi ya wagonjwa kwa mkoa huo
imepungua kwa kiasi kikubwa sana japo idadi ya wagonjwa nchini kwa ujumla
imeendelea kubakia kuwa juu.
Jumla
ya Mikoa 12 nchini iliripoti wagonjwa katika kipindi cha juma moja
lililopita ambapo mkoa wa Mara uliripoti idadi kubwa zaidi ya wagonjwa
ambayo ni 125 (Rorya 47, Musoma Mjini 40, Tarime Vijijini 26,
Musoma Vijijini 10, Butiama 2) ukifuatiwa na Dodoma 87 (Chamwino
64, Mpwapwa 17 na Dodoma mjini 6), Iringa 64 (Iringa Vijijini 63,
Mjini 1 ), Mwanza 59 (Ilemela 32, Ukerewe 19, Nyamagana 8) na Morogoro
44 (Morogoro Mjini 21, Kilosa 13, Ulanga 10). Wagonjwa waliripotiwa pia
kutoka mikoa ya Mbeya 29, Dar Es Salaam 25, Arusha 18, Kigoma
8, Rukwa 6, Simiyu 6, na Singida 2.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Wizara
bado inaendelea kukumbana na changamoto mbalimbali katika kukabiliana na
ugonjwa wa kipindupindu. Vikosi kazi vya wataalamu kutoka wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanaoendelea kuzuru maeneo
mbalimbali wameendelea kuibua changamoto hizo na kuhakikisha zinafanyiwa kazi
haraka iwezekanavyo ili kuzuia ueneaji wa vimelea vya ugonjwa huu na kisha
kuutokomeza kabisa.
Moja
ya changamoto kubwa inayoendelea kujitokeza ni pale ambapo baadhi ya wataalamu
wa afya wa ngazi mbalimbali pamoja na wanajamii wanapowaficha wagonjwa na hivyo
kutoa taarifa ya wagonjwa wachache kuliko uhalisia. Madhara yanayoambatana na
hili ni kutokuwepo kwa taarifa za kutosha zitakazoongoza juhudi za kuzuia
ugonjwa kutoka katika maeneo ambayo wagonjwa hawakutolewa taarifa, na hivyo
kuongeza hatari ya ugonjwa kuendelea kusambaa kimya kimya na baadae kusababisha
wagonjwa wengi kujitokeza katika maeneo hayo kwa mara moja.
Wizara
inaendelea kuzitaka mamlaka zinazohusika na jukumu la kutambua wagonjwa
kushirikiana na kutoa taarifa sahihi kama inavyoelekezwa katika miongozo
mbalimbali ya Wizara ikiwamo muongozo wa udhibiti wa magonjwa ya milipuko
Tanzania wa mwaka 2011 “IDSR” na muongozo wa udhibiti wa ugonjwa wa
kipindupindu toleo la tatu la mwaka 2015. Pia natoa wito kwa jamii kuwa pale
wapatapo wagonjwa wawapeleke mapema katika vituo vyetu vya kutolea huduma ili
wapatiwe matibabu sahihi na kutolewa taarifa.
Kwa
kufanya hivyo taarifa za kutosha na sahihi zitakazosaidia kupambana na ugonjwa
huu zitapatikana kwa wakati na hivyo kuwezesha kuutokomeza ugonjwa huu mapema.
Tunatoa rai kwa viongozi hususani ngazi ya Mikoa na Wilaya kutokutoa kauli za
kutaka kuwaadhibu watendaji na viongozi wa ngazi za chini kwa kigezo cha
wagonjwa wa kipindupindu kuwepo katika maeneo yao kwani kwa kufanya hivyo
wataongeza kasi ya kuficha wagonjwa na hivyo kukwamisha juhudi za kupambana na
ugonjwa huu.
Aidha
tunatoa wito kwa mikoa yote nchini kuhakikisha kuwa wanaimarisha vikao vya
Kamati za Afya ya Msingi (PHC meetings) na kutumia taarifa zinazotokana
na tathmini ya mwenendo wa ugonjwa huu katika maeneo yao ili ziwasaidie kupanga
mbinu sahihi za kuudhibiti ugonjwa wa kipindupindu.
Ndugu
waandishi wa habari,
Wizara
ilituma timu ya wataalamu kwenda Mkoani Iringa ili kufanya tathmini na kuongeza
nguvu ya kupambana na kuzuia ueneaji wa ugonjwa huu kwa wahanga wa mafuriko.
Taarifa ya tathmini hiyo imeonyesha jinsi ambavyo jitihada mbalimbali
zilizochukuliwa zinavyosaidia kuepusha madhara zaidi kwa binadamu walioathiriwa
na mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na kuepusha ongezeko la
wagonjwa wa kipindupindu katika Wilaya hiyo na maeneo jirani. Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbali
mbali itaendelea kutoa msaada wa kitaalamu kwa Mikoa na Halmashauri zote ili
kusaidia juhudi zilizopo za kupambana na ugonjwa huu nchini.
Tunaendelea
kuisihi jamii kuungana na halmashauri, mikoa pamoja na wizara katika juhudi za
kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:
- kunywa maji yaliyo safi na salama
- kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama
- kunawa mikono kwa sabuni na maji safi
- kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, maziwa na mabwawa. Tunaelewa kwamba jambo hili lina changamoto kubwa, lakini tunaisihi Mikoa na Halmashauri kuhimiza na kusimamia ujenzi na matumizi ya vyoo bora katika maeneo yao kwa kuwashirikisha wananchi.
- Kutotiririsha maji taka na vinyesi ili kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Pia
wananchi wanahimizwa kuwahi mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya mara
waonapo dalili kuu za ugonjwa wa kipindupindu ambazo ni pamoja na kuanza ghafla
kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji na kunako weza kuambatana na kutapika,
kulegea, kusikia kiu, midomo kukauka, na kuishiwa nguvu. Mgonjwa anaweza
kupoteza maisha endapo hatapata huduma yoyote ya tiba katika muda mfupi na hasa
kutokana na kuishiwa maji.
Hitimisho
Wizara
inaendelea kutoa rai kwa jamii, wataalamu na viongozi katika ngazi zote kwamba
kila mmoja wetu atimize wajibu wake katika harakati za kuudhibiti ugonjwa wa
Kipindupindu.
Aidha,
kwa mara nyingine tena tunaendelea kuwashukuru wadau wote, yakiwemo Mashirika
ya Kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika jitihada za kupambana na magonjwa
mbalimbali ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu. Aidha tunawashukuru na
kuwapongeza watumishi wa afya katika ngazi mbali mbali kwa juhudi zao katika
kupambana na ugonjwa huu. Pia tunawapongeza waandishi wa habari kwa
kuendelea kuisaidia Serikali kuielimisha jamii jinsi ya kujikinga na maambukizi
ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kusambaza taarifa mbalimbali zinazotolewa na
Wizara kwa ngazi zote zinazohusika na mapambano ya Kipindupindu.
Asanteni sana
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU UGONJWA WA KIPINDUPINDU.”
Post a Comment