Tuesday, March 1, 2016
GHARAMA ZA UMEME KUSHUKA.
Do you like this story?
SHIRIKA la Umeme (Tanesco)
limewasilisha katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) maombi ya
kushusha bei ya umeme kwa asilimia 1.1 pamoja na kuondoa kabisa gharama za
maombi ya awali ya wateja wapya na gharama za huduma kwa wateja wa majumbani.
Gharama za maombi hayo ya awali ambayo
pia yanajulikana kama gharama za fomu ni Sh 5,900 na gharama za huduma (service
charges) ni Sh 5,520 kwa mwezi kwa wateja wa majumbani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanseco, Felichesmi Mramba alisema
kuwa kisheria maombi hayo yanatakiwa kujibiwa ndani ya siku 24 ambapo wanaamini
kuwa watapata majibu mazuri.
Mramba alisema gharama za huduma
zimekuwa zikiathiri sana watumiaji wa umeme wa majumbani tofauti na wanaotumia
viwandani.
Mramba alisema kuwa maombi hayo
yamewasilishwa baada ya Tanesco kufanya tathimini ya kina kimahesabu pamoja na
kubuni namna ambayo wateja wao wataweza kupata ahueni ya gharama kwa kuzingatia
mazingira ya sasa.
Alisema punguzo hilo la asilimia 1.1 ni
kwa mwaka wa kwanza na matarajio ni kwamba mwaka wa pili, watapunguza kwa
asilimia 7.9.
“Baadhi ya vyombo vya habari
vimepotosha ukweli huo. Tunawahakikishia wananchi kuwa maombi yaliyotumwa Ewura
ni kuondoa usumbufu wanaoupata watumiaji wa umeme wa majumbani,’’ alisema
Mramba.
Alisema kwa mujibu wa sheria, Tanesco
inapotaka kubadilisha bei, iwe ni kushusha au kupandisha ni lazima iwasilishe
maombi hayo Ewura kwani ndiyo yenye mamlaka ya kisheria ya kubadilisha bei
hizo.
Alifafanua kuwa Tanseco huwasilisha
maombi yake pamoja na takwimu halisi zinazoshawishi mantiki ya kubadilishwa kwa
bei hizo na kwamba maombi yaliyowasilishwa Ewura hivi sasa, ndio ilivyotakiwa.
Aliongeza kuwa baadhi ya mambo
yanayoendana na mazingira ya sasa, ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa
umeme wa gesi, tofauti na ilivyokuwa hapo kabla. Pia alisema kuongezeka kwa
ujazo wa maji katika mabwawa makubwa hasa Mtera, kunachangia Tanesco kushusha bei hizo.
Akizungumzia
madeni ya Tanesco, Mramba alisema kuwa kiasi cha madeni yaliyotajwa na vyombo
vya habari sio sahihi.
Alifafanua
kwamba madeni hayo yamezingatiwa kikamilifu katika mapendekezo ya
kushusha bei hivyo na si kweli kwamba kushuka kwa bei kutasababisha Tanesco
kufilisika.
“Sio sahihi kusema kwamba serikali
imeilazimisha Tanesco kushusha bei ya umeme na kwamba kwa kufanya hivyo shirika
litafilisika. Tathimini tulioifanya ni ya kitaalamu na pia kwa mujibu wa sheria
ya Ewura itafanya tathimini yake kabla ya kuidhinisha bei mpya,’’ alifafanua.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ GHARAMA ZA UMEME KUSHUKA.”
Post a Comment