Saturday, March 5, 2016
MKUU WA MKOA WA MWANZA AAMURU KUKAMATWA PAPO HAPO WALIMU 8 KWA KUJIUSISHA NA MAPENZI NA WANAFUNZI
Do you like this story?
Walimu wanane
wa Shule ya Sekondari Mihama, Kata ya Kitangili, Wilaya ya Ilemela Mkoani
Mwanza, wamesimamishwa kazi, watano kati yao wakishikiliwa na polisi kwa tuhuma
za kufanya mapenzi na wanafunzi.
Pia, Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo aliyetembelea shule hiyo jana, amevunja bodi ya
shule hiyo baada ya kubainika kutofanya kikao hata kimoja tangu ilipoteuliwa
Aprili 24, 2013.
Pamoja na Mkuu
wa Shule, Joseph Malifedha, walimu wengine waliotiwa mbaroni jana ni Rodrick
Uroki, Denis Sanga, Edmund Boaz, Steven Samuel.
Walimu watatu
waliokuwa wakifundisha shuleni hapo, lakini wakahamishwa na hivi sasa wanasakwa
na polisi kwa tuhuma hizo ni Joseph Lamongi na Joeza Mzava waliohamia Sekondari
ya Sangabuye pamoja na Abdallah Mtelwe aliyehamia Tanga.
Malifedha
anadaiwa kuwachangisha fedha wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tatu kwa
ajili ya picha za kuweka kwenye vitambulisho (passport size).
Akitangaza
uamuzi huo, Mulongo alisema tume maalumu ya uchunguzi iliyoundwa Januari 27,
kuchunguza tuhuma dhidi ya walimu hao kujihusisha na mapenzi na wanafunzi
imebaini ukweli baada ya kuwahoji wanafunzi kadhaa.
“Ni
fedheha na haivumiliki kuona walimu wakifanya mapenzi na wanafunzi wao. OCD
wakamate walimu wote na uanze uchunguzi mara moja na kukusanya ushahidi
utakaowezesha wahusika kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake,” aliagiza Mulongo.
Amri hiyo
ilitekelezwa mara moja kwa walimu hao kuwekwa chini ya ulinzi.
Mulongo pia
alimwagiza Katibu wa Idara ya Utumishi wa Walimu Mkoa wa Mwanza, Genzi Sahani
kuwaandikia barua za onyo walimu wa kike shuleni hapo kwa kushindwa kulinda na
kutetea masilahi ya wanafunzi wa kike waliokuwa wakidhulumiwa kingono na walimu
wenzao kiasi cha baadhi yao kuathirika kisaikolojia.
Pia, alimwagiza
Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Khamisi Maulid kuangalia uwezekano wa kuwahamishia
shule nyingine wanafunzi waliodhulumiwa kingono na walimu wao ili kuwaepusha na
matatizo ya kisaikolojia.
Maulidi alisema
wanafunzi walioathirika zaidi ni wale wa kidato cha nne.
Katibu wa Chama
cha Walimu Tanzania (CWT), Mkoa wa Mwanza, Said Mselem alisema kitendo hicho
kimeifedhehesha taaluma ya ualimu na kuahidi kuwa ofisi yake itatanua wigo wa
uchunguzi hadi kwenye shule nyingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MKUU WA MKOA WA MWANZA AAMURU KUKAMATWA PAPO HAPO WALIMU 8 KWA KUJIUSISHA NA MAPENZI NA WANAFUNZI ”
Post a Comment