Saturday, March 5, 2016
TRA YAMDAI PROFESA TIBAIJUKA MILION 500 ZA ESCROW.
Do you like this story?
Hatima ya kesi
ya Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka kupinga kuilipa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) zaidi ya Sh500 milioni kutoka katika mgawo wa Sh1.62 bilioni
zinazohusishwa na fedha zilizochotwa Akaunti ya Tegeta Escrow, itajulikana
Machi 29, wakati Bodi ya Rufaa za Kodi (Trab) itakapotoa uamuzi.
Tarehe hiyo
imepangwa na Makamu Mwenyekiti wa Trab, Hakimu Agusta Mmbando baada ya
kukamilika kwa hatua ya usikilizwaji pande zote mbili kwenye kesi hiyo.
Profesa
Tibaijuka alikata rufaa Trab baada ya TRA kumpelekea madai ya malipo ya kodi ya
Sh586 milioni kutokana na mgawo wa Sh1.62 bilioni anazodaiwa kupokea kutokana
na fedha zilizochotwa kutoka akaunti hiyo iliyofunguliwa na Shirika la Umeme
(Tanesco) na kampuni ya kufua nishati hiyo ya IPTL kwa ajili ya kuhifadhi fedha
za malipo ya ununuzi wa umeme wakati mzozo wao ukiwa mahakamani, lakini
zikachotwa kwa njia ambayo ilizua shaka.
Rufaa hiyo
ilisikilizwa na Hakimu Mmbando Februari 17, 19 na 22 wakati Profesa Tibaijuka
alipokuwa akitoa ushahidi.
Inadaiwa kuwa
Profesa Tibaijuka, ambaye aliondolewa katika wadhifa wake wa Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na sakata hilo, aliwekewa fedha hizo
kwenye akaunti yake na James Rugemalira, Mkurugenzi wa VIP Engineering &
Marketing Limited iliyokuwa kati ya wanahisa wa IPTL.
Kutokana na
mgawo huo, Desemba 31, 2015, TRA ilimtaka alipe kodi hiyo, baada ya kushindwa
kufanya marejesho kutokana na mgawo huo.
Hata hivyo,
alipinga madai hayo na kisha akakata rufaa Trab kupinga hatua ya TRA kumtaka
alipe kiasi hicho cha kodi, pamoja na mambo mengine akidai kuwa hajawahi
kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira.
Katika rufaa
hiyo namba 22 ya mwaka 2015, Profesa Tibaijuka anadai kuwa makadirio hayo ya
TRA ya malipo ya kodi ni kinyume cha Sheria ya Kodi na hakupaswa kufanya
marejesho kwa kuwa hakupokea kipato chochote katika muda huo uliotajwa.
Akiongozwa na
wakili wake, Dk Nshalla Rugemeleza wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo,
Profesa Tibaijuka alidai kuwa fedha hizo zilikuwa ni mchango uliotolewa kwa
Taasisi ya Joha Trust, kwa ajili ya Shule ya Wasichana ya Barbro Johansson
inayomilikiwa na taasisi hiyo.
Profesa
Tibaijuka alidai kuwa yeye si mwanahisa wa taasisi hiyo, bali ni mmoja wa
wadhamini na kwamba TRA ilipuuza ushahidi wake kuwa VIP ilitoa mchango kwa Joha
Trust na yeye kama mdhamini alizipeleka Joha Trust kupitia Bank M.
Aliongeza kuwa
TRA haikuzingatia ukweli kwamba Joha Trust na yeye ni vitu viwili tofauti, huku
akisisitiza kwamba fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya Joha.
Hata hivyo,
wakili wa TRA, Noah Tito ilipinga madai ya Profesa Tibaijuka akidai kuwa
utetezi wake hauna msingi kwani fedha hizo ziliingia kwenye akaunti binafsi ya
Profesa Tibaijuka na siyo ya Joha Trust.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TRA YAMDAI PROFESA TIBAIJUKA MILION 500 ZA ESCROW.”
Post a Comment