Thursday, April 14, 2016

SERIKALI YA MAREKANI YAAHIDI KUENDELEA KUISAIDIA TANZANIA HASA SEKTA ZA AFYA NA ELIMU





Serikali ya Marekani imeihakikishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kuendeleza uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili ikiwa ni  pamoja na kutoa ufadhili na misaada mbalimbali ya miradi ya maendeleo hasa katika sekta za afya na Elimu.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari muda mfupi mara baada ya kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani hapa nchini aliyeongozana na Ujumbe wa watu 15 wanaoshughulikia miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani hapa nchini, Waziri wa Mambo ya Nje,Afrika Mashariki,Kikanda na Ushirikiano wa Kimataifa Dr Augustine Mahiga alisema kuwa licha ya kutokea kutoelewana kwa Serikali hiyo na Tanzania hivi karibuni lakini nchi hiyo imesema kuwa haitasitisha kuendeleza miradi muhimu kama vile miradi ya Elimu na Afya  iliyoanzishwa hapa nchini na Seikali ya Marekani sambasamba na kuendeleza Ushirikiano huo katika nyanja zingine za kimaendeleo.

Aidha Waziri Dr Mahiga aliwatoa hofu watanzania na kusema kuwa miradi yote ambayo ilianzishwa hapa nchini kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani itaendelezwa kama ilivyopangwa hapo awali na kuahidi miradi mingine zaidi itakayoleta tija kwa Taifa sambamba na kuleta ajira kwa Watanzania walio wengi.

Kwa Upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Mark Childress alisema kuwa upo umuhimu wa kuendeleza mahusiano kati ya Tanzania na Marekani hasa katika utoaji wa misaada mbalimbali ya kimaendeleo hivyo Serikali ya nchi hiyo itaendeleza na kukuza  mahusiano hayo licha ya changamoto mbalimbali za kisiasa zilipo nchini.

Nchi hiyo ya Marekani imeahidi kuongeza miradi mingi zaidi nchini itakayolenga kukuza uchumi wa Tanzania na kuitoa nchi hiyo katika hali ya umasikini iliyopo hivi sasa.

Katika mazungumzo hayo, pia walijadili jinsi ya kuimarisha masuala ya kidiplomasia na namna ya kuzidisa usalama wa kikanda kwa manufaa ya wote.

0 Responses to “ SERIKALI YA MAREKANI YAAHIDI KUENDELEA KUISAIDIA TANZANIA HASA SEKTA ZA AFYA NA ELIMU ”

Post a Comment

More to Read