Wednesday, August 24, 2016
WENYE VIRUSI VYA UKIMWI (VVU) SASA KUWAHISHIWA ARVs
Do you like this story?
WATU
watakaogundulika kuwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wataanza kupewa na kutumia
dawa za kupunguza makali ya ugonjwa (ARVs) bila kusubiri kinga zao za mwili
kupungua kama ilivyozoeleka.
Wakati
utaratibu huo mpya ukitarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu, kwa upande wake, Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi kupitia kwa Mwenyekiti wake,
Constantine Kanyasu, imeshauri serikali kuangalia namna ya kuruhusu dawa
ziingizwe na kuuzwa madukani kwa bei nafuu kwa ajili ya watu ambao hawako chini
ya mpango wa serikali.
Hayo
yalielezwa jana mjini Dodoma kwenye kikao cha kamati hiyo ya Bunge ambayo
ilipokea taarifa iliyofikiwa katika utafiti wa upatikanaji wa chanjo ya Ukimwi.
Katibu
Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki
Ulusubisya aliieleza kamati juu ya mabadiliko katika tiba na kusema mtu yeyote
anayepima na kugundulika kuwa ana Virusi Vya Ukimwi, ataanza kupatiwa ARVs mara
moja.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hii, Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Dk
Angela Ramadhani, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Shirika la
Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) yaliyotolewa mwaka jana baada ya tafiti
kubainisha kuwa zipo faida za kuwahi kupata dawa husika.
Dk
Ramadhani alisema maagizo hayo ya WHO yanatokana na tafiti zilizofanyika katika
nchi mbalimbali na kubainisha kuwa kutumia ARVs kabla ya kinga ya mwili
kushuka, kuna faida kutokana na kuonesha kuwa kunakuwa na usalama zaidi.
Kwa
mujibu wa Dk Ramadhani, baada ya mwongozo kutolewa mwaka jana, Aprili mwaka
huu, shirika hilo liliita nchi wanachama na kusambaza taarifa hizo kwa ajili ya
kuziwezesha kujipanga kiutekelezaji.
“WHO
wakishatoa mwongozo, huita wataalamu na kuwaeleza ili nchi zijiendae. Kwa
mfano, kama zina uwezo wa kutoa dawa hizo,” alisema Dk Ramadhani na kusema pia hapa nchini,
wameanza wiki hii kupitia miongozo ya zamani kabla ya utaratibu huo mpya kuanza
Oktoba mwaka huu.
Wakati
huo huo, wakati wa kikao na Kamati ya Bunge baada ya wizara kuonesha kuwa uwezo
wa serikali wa kutoa dawa hizo unaishia kwa watu milioni 1.3 licha ya kuwa na
watu 2.4 wenye VVU, Mwenyekiti wa Kamati, Kanyasu alishauri suala hilo liangaliwe
kwa umakini.
“Kama
uwezo wa serikali unaishia kwa watu milioni 1.3, ni kwa nini serikali isijikite
hawa wanaopata free (bure) halafu hawa private (binafsi) wakaruhusiwa kuingiza
dawa zikauzwa kwenye maduka kwa bei nafuu ili mtu akishajiona ana Ukimwi aende
akanunue ili kuziba pengo hilo la watu milioni 2.4,” alihoji Kanyasu wakati akizungumza na
waandishi wa habari.
Katika
kikao hicho cha kamati na watendaji kutoka wizara, taarifa zilibainishwa kwamba
wafadhili wamepunguza na wanaendelea kupunguza bajeti katika masuala ya Ukimwi.
Kuhusu
chanjo, ilielezwa na Katibu Mkuu kwamba, shughuli zote zilizopangwa awali
kuhusu chanjo zilisitishwa Juni, 2015 baada ya fedha kutoka kwa wafadhili
kwisha jambo ambalo serikali imechagizwa kutoa fedha uendelee.
Ilisisitizwa
kwamba Tanzania inapaswa ijikite kwenye chanjo ikizingatiwa kwamba haiwezi
kutegemea tafiti za mataifa mengine kutokana na wadudu kutofautiana.
Wakati
huo huo, kamati ilielezwa changamoto zilizopo kwenye utafiti juu ya suala la
Ukimwi kwamba Watanzania wengi wanaogopa kuwekewa vimelea vya kupambana na
Ukimwi wakidhani wakipandikiziwa watakuwa wameambukizwa. Katibu Mkuu alisema
hali hiyo inasababisha watafiti kupata shida ya kupata watu wa kufanyia
utafiti.
Awali,
katika taarifa yake kuhusu utafiti wa chanjo ya Ukimwi, Katibu Mkuu alisema
wizara yake kupitia Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili na Taasisi ya Taifa ya
Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Kituo cha Mbeya zilifanya utafiti mwaka
2014.
Alisema
kati ya Februari 2007 na Februari 2008, watu 162 miongoni mwa 177 walifanyiwa
uchunguzi na chanjo kuonesha usalama mzuri na hakukuwa na madhara makubwa
yanayohusiana moja kwa moja na chanjo.
Aidha,
asilimia 100 ya washiriki waliopata chanjo halisi waliweza kutengeneza kinga
zinazohusisha seli za kinga ya mwili na protini zilizoko kwenye damu dhidi ya
VVU. Kutokana na mafanikio ya awamu ya kwanza, mradi wa awamu ya pili
ulifanyika Tanzania na Msumbiji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “ WENYE VIRUSI VYA UKIMWI (VVU) SASA KUWAHISHIWA ARVs”
Post a Comment