Friday, February 24, 2017

MAWAZIRI 15 WA SADC KUJADILI SAKATA LA WATANZANIA WALIOFUKUZWA MSUMBIJI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga, amesema anatarijia kulifikisha suala la watanzania wanaofukuzwa nchini Msumbiji kwa kosa la kuingia na kufanya kazi nchini humo kinyume cha sheria za uhamiaji za nchi hiyo katika mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi mwanachama wa SADC unaotarajia kufanyika kesho jijini Dar es Salaam kupitia kamati yake ndogo ya siasa na demokrasia.
Mahiga ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa ili kuhakikisha watanzania wanarejea nchini salama pamoja na mali zao, ni lazima wizara yake ifanye mazungumzo ya kidiplomasia na wizara husika ya Msumbiji ili waruhusiwe kupata mali walizochuma nchini humo kutokana kwamba baadhi walizipata kinyume cha sheria kwa kuwa wengi wao hawakuwa na vibali halali vya kazi na makazi.
“Si sahihi kuhalalisha kisicho sahihi. Usalama wao upo ila mali walizochuma huko zinaweza kuwa haramu kama sheria ikifuatwa sababu hawakuwa na kibali cha kazi, katika mkutano huo ambao mimi ndio mwenyekiti wake tutazungumza na wenzetu maana waziri wa Msumbiji atakuwepo ili kuona jinsi gani mali walizochuma huko watazipata na kurudi nazo au waziuze huko huko ili wapate pesa,” amesema.
Kuhusu mkutano, Mahiga amesema mawaziri wa mambo ya nje kumi na tano wa nchi mwanachama wa SADC wanatarajia kuhudhuria katika mkutano humo.
Aidha, Dkt. Mahiga amesema kuwa wizara yake inawasiliana na idara ya uhamiaji mkoa wa Mtwara kuhakikisha kwamba hakuna raia wa kigeni watakao ingia nchini  kwa kutumia mgongo wa watanzania waliofukuzwa nchini humo.

0 Responses to “ MAWAZIRI 15 WA SADC KUJADILI SAKATA LA WATANZANIA WALIOFUKUZWA MSUMBIJI”

Post a Comment

More to Read