Tuesday, March 11, 2014

AFRIKA KUSINI YAWATIMUA MABALOZI 3 WA UBALOZI WA RWANDA NCHINI HUMO....RWANDA NAYO YAJIBU MAPIGO KWA KUWATIMUA MAOFISA 6 WA UBALOZI WA AFRIKA KUSINI.




SERIKALI ya Rwanda, imefukuza maofisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini muda mfupi baada ya nchi hiyo kuwataka maofisa  watatu ubalozi wa Rwanda kuondoka Afrika Kusini.
 
Aidha, kutokana na hatua hizo, Afrika Kusini imeanza kuangalia uwezekano wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Rwanda, kutokana na mvutano wa siku za hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili, uliosababisha kila upande kufukuza maofisa ubalozi.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo amethibitisha Serikali yake kuwafukuza maofisa sita wa Ubalozi wa Afrika Kusini, kwa madai kuwa Serikali ya Afrika Kusini imewa hifadhi waasi waliojihusisha na mashambulizi ya kigaidi.
 
“Tumewafukuza wanadiplomasia sita wa Afrika Kusini kuwajibu na pia ni kutokana na wasiwasi wetu kuwa nchi hiyo inawahifadhi waasi ambao wanahusika na mashambulizi ya kigaidi nchini Rwanda,” amesema waziri huyo.
 
Afrika Kusini ilichukua hatua hiyo ya kuwafukuza maofisa wa Rwanda, baada ya nyumba ya mpinzani wa Rwanda, Jenerali Kayumba Nyamwasa anayeishi Afrika Kusini kushambuliwa mapema wiki iliyopita jijini Johannesburg.
 
Gazeti la Sunday Times nchini Afrika Kusini, lilinukuu chanzo cha habari kutoka kitengo cha diplomasia, kikibainisha kuwa Afrika Kusini wanaangalia uwezekano wa kumrudisha nyumbani Balozi wao aliyeko Kigali.

0 Responses to “AFRIKA KUSINI YAWATIMUA MABALOZI 3 WA UBALOZI WA RWANDA NCHINI HUMO....RWANDA NAYO YAJIBU MAPIGO KWA KUWATIMUA MAOFISA 6 WA UBALOZI WA AFRIKA KUSINI.”

Post a Comment

More to Read