Thursday, March 27, 2014

BUNGE LA KATIBA LIVUNJWE KIKWETE AMEMALIZA KAZI.




Siasa ni kama mchezo ambao kanuni zake zinaweza kuitofautisha na soka; mchezo ambao hauhitaji waamuzi watatu uwanjani ili uchezeshwa kwa haki.

Haishangazi, hata hivyo kuona siasa ikiitwa mchezo mchafu ambao kanuni za uchezeshaji wake ndizo zinazoweza kuibua hisia zikiwamo za kutokuwapo kwa haki katika uchezeshaji wake.

Mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya nchini ambao ulianza Aprili 6, 2012 kwa  Rais Jayaka Kikwete kutangaza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba ikiwa ni kutekeleza ahadi yake kwa Watanzania kuwa angewapatia Katiba Mpya umefikia patamu, ingawa umeacha pia maswali mengi.

Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma wiki jana lilishuhudia mambo kadhaa ambayo yameacha wengi vinywa wazi.

Kitu kisichotarajiwa na kilichowashangaza wengi ni Rais Kikwete kuhutubia Bunge hilo Ijumaa akiwa tayari na majibu ya baadhi ya vipengele vya Rasimu ya Pili ya Katiba mkononi mwake ikiwamo muundo wa Muungano.

Kutokana na hotuba hiyo, inawezekana Rais Kikwete hakuwa tayari kupokea maoni tofauti na msimamo wake na chama chake, CCM ambao ni serikali mbili.

Kwa upande wao, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanahoji kama ni hivyo, ilikuwaje Kikwete akatumia Sh75 bilioni za kodi za Watanzania  kuandaa mchakato ambao tayari alikuwa na  majibu yake?

Msomi na mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho anasema Rais Kikwete ‘ametibua’ mwenendo wa mchakato kwani kama alikuwa ana hoja zake, alitakiwa kutumia nafasi yake kujadiliana na tume hiyo badala ya kutoa maoni yake mbele ya Bunge hilo.

“Alitakiwa kusimama kama mkuu wa nchi kuwa tofauti na msimamo wowote kwa kutoa mwelekeo wa kuchambua rasimu badala ya kutoa maoni yake, kufanya hivyo ni kupinga wazi kwamba kilichopendekezwa ndani ya rasimu ni makosa,” anasema na Profesa Shumbusho.

“Kutokana na hotuba hiyo sioni haja ya kuendelea na mchakato huo, kama serikali mbili ndiyo zinahitajika kwa hivyo ni vyema Bunge livunjwe na tuanze upya mchakato, vinginevyo hakuna kitakachoendelea”.

Kwa upande wake,  Profesa Bonaventure Rutinwa kutoka Shule Kuu ya Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema tatizo lililojitokeza katika uwasilishaji wa hotuba ile ni pamoja na kujenga dira na imani ya mawazo yake kuwa ni sahihi, hivyo kuathiri uhuru na mawazo ya wajumbe waliyokuwa nayo awali.

0 Responses to “BUNGE LA KATIBA LIVUNJWE KIKWETE AMEMALIZA KAZI.”

Post a Comment

More to Read