Thursday, March 27, 2014
SEIF: HATUKO TAYARI KUJADILI SERIKALI MBILI.
Do you like this story?
Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake cha CUF hakiko tayari
kujadili mfumo wa Muungano wa serikali mbili kama inavyotetewa na wabunge wa
CCM na Rais Jakaya Kikwete.
Amesema tayari amewaandikia barua Rais
Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuwaeleza juu ya msimamo huo.
Maalim Seif alitoa msimamo huo jana kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti mjini Unguja.
Isitoshe, amesema CUF imebaini kuwa kuna
njama za kufuta kipengele katika Katiba ya Zanzibar kinachosema; “Zanzibar ni
nchi” na kwamba hiyo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa kuwa Wazanzibari
kamwe hawatakubali kufanya hivyo.
Maalim Seif amesema haikuwa mwafaka kwa Rais
Kikwete kukosoa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba yanayotaka mfumo wa Muungano
kuwa wa serikali tatu.
Amesema Jaji Warioba aliweka kando itikadi
yake ya CCM katika utendaji wake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuja na
uamuzi huo kwa vile ndiyo tiba ya kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Mapendekezo yaliyowasilishwa na Jaji Warioba
hayakuwa maoni yake, yale ni maoni ya wananchi, Tanganyika imevaa koti la
Muungano, ametoa ushahidi wake ili kujenga mwafaka katika kuendeleza Muungano
wenye mfumo wa serikali tatu,” alisema Maalim Seif.
Alisema Muungano wa serikali mbili
hauvumiliki na kama kuna watu wanaendelea kuutetea mfumo huo, Zanzibar inaweza
kutumia sheria yake ya kura ya maoni kuwauliza wananchi wanaotaka na wasiotaka
jambo hilo.
“Nimemwandikia barua Rais Kikwete, nakala
nimempelekea Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Tanzania Bara wanataka
Zanzibar iondoe kifungu cha Katiba kinachosema Zanzibar ni nchi, jambo hilo
halitapita...tutafanya kampeni wananchi walikatae,” alieleza Katibu Mkuu huyo
wa CUF.
Alisema ni jambo la kusikitisha katika hotuba
yake alijisahau kama ni mkuu wa nchi na analihutubia Bunge Maalumu badala yake
akaegemea kuwa mwenyekiti wa CCM.
Alisema haikuwa sahihi kutoa vitisho na
kutaja ikiwa Serikali ya Muungano chini ya Serikali tatu italegalega, jeshi
litachukua madaraka ya nchi.
“Rafiki na ndugu yangu Kikwete, usifikiri huu
ni wakati ule wa Julius Nyerere, akisema yeye hakuna wa kumpinga. Mambo
yamebadilika, usijifanye ni Nyerere mpya, hakuna atakayekusikiliza na
kubabaika,” alisisitiza Maalim Seif.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SEIF: HATUKO TAYARI KUJADILI SERIKALI MBILI.”
Post a Comment