Thursday, March 27, 2014
KUNA NJAMA KUVURUGA BUNGE.
Do you like this story?
Kuna njama. Maneno haya mawili ndiyo
yametumiwa na pande mbili zinazopingana ndani ya Bunge Maalumu la Katiba,
kuelezea hali iliyojitokeza jana wakati wa kikao cha Bunge hilo kuhusu mvutano
wa mabadiliko ya kanuni.
Njama zinazoelezwa na pande hizo ni za
kuvuruga mchakato wa Katiba Mpya, zikirejea yaliyotokea jana jioni ikiwamo
zomeazomea hali iliyomlazimu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel
Sitta kuliahirisha Bunge hadi leo jioni.
Baada ya kuahirisha Bunge hilo, Sitta
alikutana na waandishi wa habari na kusema kwamba kuna njama za baadhi ya
wanasiasa kutumia vurugu kuhujumu mchakato wa upatikanaji wa Katiba, badala ya
kujenga hoja.
Bila kuwataja wanasiasa hao, Sitta alisema
ikiwa hawataki kuendelea na mchakato huo, basi waondoke na kuwaacha wenye nia
njema.
“Wanasiasa hawa wamedhamiria kuvuruga
mchakato wa Katiba, tuhuma ambazo tumetuhumiwa leo na Lissu (Tundu) ni uongo na
uzushi, mimi sihusiki na kupeleka marekebisho ya kanuni kwenye Kamati ya Kanuni
na Haki za Bunge,” alisema Sitta.
Sitta alikuwa anajibu mchango wa mjumbe wa
Bunge, Tundu Lissu alioutoa mapema kwenye kikao cha jioni, akipinga
kilichoelezwa ni njama za kutaka kubadili kanuni kinyemela ili kumsaidia
mwenyekiti kulidhibiti Bunge.
Sitta amesema kwa kuzingatia kanuni ya 59
(1), Kamati ya Uongozi ina mamlaka ya kupeleka marekebisho ya kanuni ili
kuliwezesha Bunge kufanya kazi vizuri.
Amesema hoja kwamba haiwezekani kufanyika
mabadiliko hata kabla ya kuanza kutumika kanuni, siyo ya msingi kwani kila kitu
kinabadilika kutokana na mazingira yake.
“Kamati ya Uongozi ndiyo ilipeleka waraka wa
mabadiliko ya kanuni kwa Kamati ya Kanuni na Haki kwa kuzingatia kanuni, lakini
hata kabla ya kujadiliwa na kamati husika inaonekana kuna wajumbe ndiyo
wameichukua na kuifikisha bungeni,” alisema Sitta.
Alisema kwa kiasi kikubwa marekebisho ambayo
yangesomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, yalilenga kutoa
ufumbuzi wa kanuni ya 37 na 38 juu ya upigaji kura ama uwe wa wazi au siri.
Sitta alisema pamoja na hilo, kulikuwa na
marekebisho ya msingi kama kuweka utaratibu mzuri wa majadiliano katika kamati
pia kuweka utaratibu wa vikao vya Bunge kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “KUNA NJAMA KUVURUGA BUNGE.”
Post a Comment