Thursday, March 6, 2014
GESI NYINGI ZAIDI YAGUNDULIKA BAHARI KUU TANZANIA.
Do you like this story?
Kampuni ya Statoil na mshirika wake, Exxon Mobil,
imetangaza matokeo mazuri ya majaribio ya gesi kwenye kitalu namba mbili katika
kina kirefu cha bahari kisima cha Zafarani-2.
Kwa mujibu wa Meneja wa Statoil Tanzania, Oystein Michelsen, majaribio hayo kwenye kisima cha Zafarani-2, kimeonyesha kuwa na uwezo wa kutiririsha futi za ujazo milioni 66 kwa siku.
Amesema takwimu zilizopatikana kwenye majaribio hayo, ni muhimu kwa ajili ya kupunguza shaka inayoweza kuwapo siku za usoni kuhusu gesi iliyoko ya kina kirefu cha bahari na gesi ya kusindikwa hapa nchini.
Alifafanua kuwa majaribio ya uchimbaji yalifanywa katika kisima cha Zafarani-2 urefu wa mita 2,400 ndani ya kina kirefu cha bahari na ikiwa ni umbali wa kilomita 80 kwenda nchi kavu.
Alieleza kuwa baada ya majaribio ya kisima cha Zafarani-2 , kutafuatia uchunguzi wa kiwango cha gesi kwenye kisima cha Zafarani-3, ambacho ndicho cha mwisho kwenye utafiti katika hifadhi ya gesi kwenye kitalu namba mbili.
Amesema kutangazwa kwa matokeo ya majaribio ya kisima cha Zafarani-2 kunafuatia ugunduzi kwenye kisima cha Mronge-1 kulikofanyika Desemba 2013, ambako kunafanya ugunduzi huo kuwa kisima cha tano kwa utafiti unaofanyika kwenye kitalu namba 2.
Amesema ugunduzi huo umefanya jumla ya kiasi cha gesi iliyogundulika kufikia futi za ujazo wa kati ya trilioni 17-20 (Tcf).
Amesema kabla ya ugunduzi uliotokea kwenye kisima cha Mronge-1 kulikuwa na ugunduzi mkubwa gesi wakati wa uchimbaji wa awamu ya kwanza kwenye kisima cha Tangawizi-1, Zafarani-1 na Lavani-1, na ugunduzi mwingine kwenye kisima cha Lavani-2.
Kampuni ya Statoil ina leseni ya kufanya utafiti katika kitalu namba mbili kwa niaba ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ikiwa na asilimia 65 wakati mbia wake kampuni ya ExxonMobil Exploration and Production Tanzania Ltd ikichukua asilimia 35.
Kampuni ya Statoil imekuwa Tanzania tangu mwaka
2007, ilipopewa leseni na serikali kwa ajili ya kufanya utafiti kwenye kitalu
namba 2.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “GESI NYINGI ZAIDI YAGUNDULIKA BAHARI KUU TANZANIA.”
Post a Comment