Sunday, March 9, 2014
IKULU YAKANUSHA HABARI YA GAZETI LA MWANANCHI YA RAIS KUMTEMBELEA MFUNGWA MARANDA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI.
Do you like this story?
Ndugu Margaret Chambili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). |
Gazeti la Mwananchi la leo,
Jumapili, Machi 9, 2014, kwenye ukurasa wake wa tano, limechapisha habari zenye
kichwa cha habari –“JK awatembelea Maranda, Mkambala Hospitali ya Taifa
Muhimbili.” Katika habari hiyo, Gazeti hilo limeripoti: “Rais Jakaya Kikwete
jana alimtembelea mfungwa, Rajab Maranda anayetumikia kifungo cha miaka 18
gerezani kwa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
akisumbuliwa na tatizo la mgongo.” Habari hizi ni uongo.
Mhe. Rais hakumtembelea Ndugu
Maranda jana (Jumamosi) kama ilivyoripotiwa na gazeti hili na wala hajawahi
kumtembelea siku yoyote iwe ni hospitalini ama kwingineko. Kwa hakika, ni jambo
la kusikitisha kuwa Gazeti lenye heshima na hadhi kama Mwananchi linaweza
kujiingiza katika utunzi na uandishi wa uongo wa kiasi hiki.
Ukweli wa mambo yaliyotokea jana ni kama
ifuatavyo: Ni kweli Mhe. Rais alitembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji
wa Mishipa ya Fahamu (MOI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana
(Jumamosi). Alikwenda kuwajulisha hali wanahabari wawili – Ndugu Salum Mkambala
wa Channel Ten na Margaret Chambili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Mhe.
Rais alianza kumtembelea Ndugu Mkambala ambaye amelazwa wodi binafsi –Private
Ward – D, kufuatia ajali ya gari iliyomfika kwenye eneo la Visiga, Mkoa wa
Pwani, akiwa njiani kwenda Morogoro mwishoni mwa wiki. Chumba hicho kilikuwa na
wagonjwa watatu. Baada ya kuzungumza na Mkambala, Mhe. Rais, kama ilivyo
kawaida yake anapotembelea wagonjwa hospitali, aliwasalimia na kuwajulia hali
wagonjwa wengine wawili ambao wako katika chumba hicho kimoja na Ndugu
Mkambala.
Wagonjwa hao wawili ni Ndugu John Mhina,
ambaye huko nyuma alipata kusoma na Mhe. Rais na Ndugu Reuben Nyanga. Baada ya
kumaliza kuwajulisha wagonjwa hao wa Private Ward D, Mhe. Rais alikwenda kwenye
wodi nyingine binafsi – Private Ward K – ambako alimjulia hali Ndugu Margaret
Chambiri ambaye ni mgonjwa pekee aliyelazwa katika chumba hicho.
Baada ya hapo, Rais Kikwete aliondoka
Muhimbili kurudi Ikulu, Dar Es Salaam. Hakuna wakati wowote, Mh. Rais
alimtembelea Ndugu Maranda ama mgonjwa mwingine kwenye Hospitali hiyo ya
Muhimbili. Ni matarajio ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, kuwa Gazeti
la Mwananchi na wahariri wake, watakuwa wakweli kwa nafsi zao wenyewe na
watakuwa na busara ya kutosha kusahihisha makosa haya kwa misingi ya taaluma ya
uandishi wa habari ambayo ni dhahiri wanaijua fika.
Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais, Ikulu, DAR ES SALAAM. 09 Machi, 2014 Rais Jakaya Mrisho Kikwete
alipotembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI)
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana (Jumamosi) kuwajulia hali
wanahabari wawili – Ndugu Salum Mkambala wa Channel Ten (juu) na (chini) Ndugu
Margaret Chambili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ IKULU YAKANUSHA HABARI YA GAZETI LA MWANANCHI YA RAIS KUMTEMBELEA MFUNGWA MARANDA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI.”
Post a Comment