Friday, March 28, 2014

MCHAKATO KUMNGO”A SPIKA EALA WAANZA.




 Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) wameanza rasmi mchakato wa kumwondoa madarakani spika wao, Margareth Zziwa kutoka Uganda baada ya kuwasilisha hati ya kusudio hilo kwa katibu wa bunge hilo, Kenneth Madete.

Habari zilizotufikia na kuthibitishwa na katibu wa Bunge la Eala, Keneth Madete zinaeleza kuwa hati hiyo inayotoa fursa kwa hoja hiyo kuwasilishwa rasmi bungeni, iliwasilishwa juzi asubuhi.
“Huenda hoja hiyo ikajadiliwa Jumanne ijayo,” alisema Madete baada ya kuthibitisha kuwa ofisi yake imepokea barua hiyo.

Baadhi ya wabunge waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao,  walisema barua hiyo imewasilishwa baada ya kufuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kusainiwa na wabunge wanne kutoka kila nchi.

“Kikanuni tumewasilisha kusudio la hoja ya kutokuwa na imani na spika kwa muda usiopungua Saa 24, kabla ya hoja hiyo kuwasilishwa rasmi na tayari tumetekeleza hilo leo (juzi), asubuhi,” alisema mmoja wa wabunge hao.

Kwa mujibu wa kanuni, hati hiyo inatakiwa kusainiwa na wabunge wasiopungua wanne kutoka kila nchi mwanachama; EAC inaundwa na nchi tano za Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi na Rwanda,  ambapo kila nchi huwakilishwa na wabunge tisa na hivyo kufanya idadi yao kuwa 45.

Mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania, Adam Kimbisa alisema hadi sasa yeye binafsi na kwa nafasi yake kama kiongozi wa wenzake hajapata taarifa rasmi kuhusu kusudio hilo wala ombi la kusaini hati ya kumng’oa spika.

Ofisa habari na mawasiliano ya Umma wa Eala, Bobi Odiko alisema hadi jana bado hakuwa amepata taarifa rasmi ya mkakati huo ingawa alikiri kuzisikia. Katibu wa bunge hilo, Kenneth Madete hakupatikana jana kuzungumzia suala hili baada ya kutokupatikana ofisini kwake wala kwa njia ya simu.

Pamoja na mambo mengine, wabunge wa Eala wanapanga kumng’oa spika wao kwa madai ya kushindwa kumudu majukumu yake, upendeleo kwenye safari za nje miongoni mwa wabunge,  ambapo baadhi wanajirudia katika ziara huku wengine wakiambulia safari chache.

Zziwa, ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo ndani ya EAC, pia anatuhumiwa kupachika ndugu zake kwenye timu ya Bunge la Uganda na kulipwa posho wakati wa michezo ya kibunge iliyofanyika jijini Kampala mwishoni mwa mwaka jana.
Spika wa kwanza wa Eala alikuwa Abdulrahama Kinana wa Tanzania, aliyefuatiwa na Abdirahim Abdi kutoka Kenya aliyepokewa na Ziwa.

0 Responses to “MCHAKATO KUMNGO”A SPIKA EALA WAANZA.”

Post a Comment

More to Read