Thursday, March 13, 2014

SITTA AJA NA FALSAFA YA CHURA.




Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amechaguliwa kwa kishindo kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba, huku akisema kuchaguliwa kwake ni sawa na kumrudisha chura kwenye dimbwi la maji.


Jana, Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alipata kura 487 na kumbwaga mpinzani wake, Hashimu Rungwe wa Chama cha Ukombozi wa Umma aliyepata kura 69.


Wajumbe wengine, Dk. Terezya Huvisa pia wa CCM na John Chipaka wa Tadea, walijitoa katika kinyang’anyiro hicho ambacho tangu awali Sitta alionyesha kujiandaa kwa kutengeneza vipeperushi alivyovisambaza kwa wajumbe kama sehemu ya kujinadi.


Akizungumza na wajumbe ambao muda mwingi walikuwa wakimshangilia, Sitta alionekana kujiamini kabla na baada ya uchaguzi. Pia alitumia misemo lugha ya picha ikiwamo ya chura kuishi majini, akimaanisha kuwa wajumbe wamemchagua mtu mwenye uwezo, uzoefu na weledi wa kuongoza shughuli za Bunge.


“Jamani kunichagua mimi ni kama kumrejesha chura kwenye dimbwi la maji alilolizoea. Msiwe na wasiwasi ataogelea tu na ninawaahidi kuwa ikiwa kwa kudra za Mwenyezi Mungu, mtanichagua nitawatumikia kwa uaminifu, sitakubali upendeleo wa aina yoyote, nitasimamia kanuni tulizozipitisha hapa,” amesema.
Aliongeza kusema: “Nitawaongoza kwa utumishi uliotukuka na uadilifu ili tupate Katiba bora, yenye viwango na kwa wakati.

0 Responses to “SITTA AJA NA FALSAFA YA CHURA.”

Post a Comment

More to Read