Monday, April 28, 2014
MASHAMBA YA BALALI KUGAWANYWA KWA WANANCHI.
Do you like this story?
Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero
imeamua kufuta miliki ya mashamba yote makubwa yasiyoendelezwa na taratibu mpya
zinafanyika ili kuyamilikisha kwa wananchi.
Kati ya mashamba hayo, matatu ni ya
aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Daudi Balali na
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba, Marehemu Priva Mtema yaliyoko katika
vijiji vya Lungungole na Merera ambayo wananchi wameshayavamia na kuendeleza
shughuli za kilimo.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la
Madiwani la Halmashauri ya Kilombero juzi, Mwenyekiti wake, David Ligazio
alisema taratibu za kuomba hatimiliki za mashamba hayo zifutwe zinaendelea.
Ligazio alisema wamiliki wa mashamba
hayo wameshapewa notisi na orodha yao imeshawasilishwa kwa Kamishna wa Ardhi
ili aridhie kufutwa kwa hati za mashamba hayo.
Alisema uamuzi wa kuyataifisha umekuja
baada ya halmashauri kubaini kuwa yamekuwa hayaendelezwi na hivyo kusababisha
maeneo hayo kuwa misitu wakati wananchi wanahitaji maeneo ya kulima.
Alisema ukaguzi wa kumbukumbu
umeonyesha kuwa idadi kubwa ya wamiliki hao hawapo wilayani Kilombero na maeneo
hayo yanamilikiwa kwa hati za muda mrefu bila kufuata taratibu.
Alisema utaratibu unaofanyika sasa ni
kuwaagiza watendaji na wenyeviti wa vijiji, kuanisha ukubwa halisi wa mashamba
hayo ili kurahisisha kazi ya kuyagawa kwa wananchi katika siku zijazo.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema taarifa
hiyo haijafika ofisini kwake, lakini akabainisha kuwa kuna watu wengi
wanaomiliki ardhi kubwa mkoani Morogoro bila kuwa na hatimiliki wala kufuata
taratibu huku wakiwa wanawatisha wananchi.
Aliwataka wananchi hao kujisimamia,
waondoe unyonge na kuzingatia taratibu za ardhi, kwamba inatakiwa kugawiwa
kupitia mkutano mkuu wa kijiji, vinginevyo wana haki ya kujitwalia maeneo hayo
na kufanya maendeleo mengine.
“Kuna matukio unakuta mtu anakaa na
mwenyekiti wa kijiji na kujifungia, wanajadili wenyewe na kugawiana maeneo ya
kijiji bila kuwashirikisha wananchi, hawa wananchi wanatakiwa kukataa hali
hiyo,” alisema.
Mwenyekiti
wa halmashauri aliyataja maeneo mashamba yanayotakiwa kugawanywa kwa wananchi
na ukubwa wake katika mabano kuwa ni Lungongole (ekari 375) na Merea (ekari
373). Pia kuna shamba lenye ukubwa wa hekta 887 linalomilikiwa na Balali, ekari
491 zinazomilikiwa na George Teni katika Kijiji cha Kisegese na ekari 500
zinazomilikiwa na Aloyce Lyenga katika Kijiji cha Idete.
Katika orodha hiyo pia kuna ekari
30,000 za Kampuni ya Merera Plantation Ltd katika Kijiji cha Merera.
Mashamba mengine ni ekari 102 za
Abdallah Sajiri zilizopo Kining’ina, ekari 295 za Peter Warwic zilizopo Lumemo,
ekari 484.9 za Sadru Meghji zilizopo Msolwa Ujamaa, ekari 120 za Ranifa EC
&DEV. Group zilizopo Kisegese na hekta 5,128 za Rubada zilizopo Ngalimila.
Ligazio alitaja mashamba mengine kuwa
ni ekari 2,390 za kampuni iliyokuwa ya usafirishaji mkoani Morogoro zilizopo
Mbingu, ekari 875 za Jerome Mwakifuna zilizopo Idete, ekari 656 za Priva
Mtemanyanja zilizopo Lungongole na ekari 1,500 za Ngwasi River Valley Inv.
zilizopo Mlimba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MASHAMBA YA BALALI KUGAWANYWA KWA WANANCHI.”
Post a Comment