Saturday, April 26, 2014

MWAMBUSI: KOCHA BORA LAZIMA AJIAMINI NA KUZINGATIA FALSAFA YAKE.




KOCHA wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi  amesema kuwa kuwaamini vijana katika klabu  kunahitaji kuwapa muda ili kufikia malengo.
Mwambusi amesema kuna mambo mawili yanatakiwa kuzingatiwa katika falsafa za mpira.
Mosi; falsafa ya mpira huwezi kuwajumuisha makocha wote kwasababu kila mtu ana falsafa yake.
Pili; kila klabu inakuwa na falsafa yake, hivyo inahitaji kocha atakayeiweza .

Mwambusi aliendelea kufafanua kuwa klabu inapokuwa na falsafa yake, mfano kutumia soka la vijana, lazima inakuwa na falsafa mbadala ili kama itashindikana mpango A basi waende mpango B.
Kocha huyo alisema si jambo la ajabu kuona timu inabadili mfumo wa soka lake ndani ya msimu mmoja, lakini inategemeana na malengo ya klabu.

Akizungumzia falsafa kwa Makocha, Mwambusi alisema kuna changamoto kubwa kwa walimu wa kitanzania kwasababu huwa hawajiamini katika mifumo yao.
“Kama viongozi wanataka mageuzi na mwalimu akakubali mageuzi bila kuzingatia mfumo wake, basi mwalimu naye atakuwa amefeli”.

“Mwalimu anatakiwa kushikilia msimamo wake na kuwaambia viongozi kuwa kama wanataka mfumo wao, basi watafute mwalimu mwingine atakayeweza kufanya kazi hiyo”.
“Mwalimu lazima uwe na msimamo na usifanye kazi kwa kushinikizwa na watu fulani”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi alibaanisha kuwa walimu wengi wa Kitanzania wanashindwa kujiamini kwasababu hawaaminiwi.;
“Viongozi wanafanya kazi kwa mazoea. Kila unachokifanya kocha wa Kitanzania wanapuuzia. Hii inatokana labda na kutuzoea”.
“Inafika muda viongozi wanaona wachukue makocha wa kigeni kwa kuamini watapata kitu fulani, lakini inakuwa tofauti”.

“Walimu wote tunasoma mpira kinadharia kama wenzetu, lakini linapofika suala la falsafa ni msimamo wa mwalimu mwenyewe”.
“ Kikubwa viongozi watuamini na kuona kama tunaweza kufanikisha malengo ya klabu zetu”. Alisema Mwambusi.
Kocha huyo alifanikiwa kuipa nafasi ya tatu Mbeya Cit fc msimu huu kwa kufikisha pointi 49 alisema kwa upande wake ana msimamo mkali na anaamini katika vitu vyake.
“Siku zote nina falsafa yangu na ninaiamini sana. Siwezi kuibadili bila kujali nitapoteza kazi”. Alisema Mwambusi.
Pia Mwambusi amewaomba makocha wenzake kutumia muda wao mwingi kulea vipaji vya wachezaji vijana.
“Isiwe kuwafundisha tu jinsi ya kupiga mpora. Pia tujikite katika masuala ya nidhamu, ndani na nje ya uwanja”.
“Saikolojia nayo lazima ipewe kipau mbele kwa wachezaji vijana ili kuwajenga katika misingi bora”. Alisema Mwambusi.

Aidha, aliwataka viongozi wa klabu kuwajibika katika majukumu yao ili kuwaweka wachezaji katika mazingira mazuri hususani mishahara na posho zao.
“Mpira unahitaji sana saikolojia. Hata aje Messi au Ronaldo hapa, halafu akafiwa na mama yake na umwambie tutakupa milioni 10 cheza mechi hii tu, sidhani kama atacheza vizuri”.

“Maslahi ni muhimu, lazima wachezaji wapate fedha zao mwisho wa mwezi. Viongozi wajipange kufanya vitu vya msingi kwa wachezaji”. Alisisitiza Mwambusi.

0 Responses to “MWAMBUSI: KOCHA BORA LAZIMA AJIAMINI NA KUZINGATIA FALSAFA YAKE.”

Post a Comment

More to Read