Wednesday, April 2, 2014

PLUIJM: WACHEZAJI YANGA WAZEMBE.




Dar es Salaam.  Kocha wa Yanga, Hans der  Van Pluijm amesema uzembe wa baadhi ya wachezaji wake unaigharimu timu hiyo katika harakati zake za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu; huku akiwataka washambuliaji wake kubadilika.

Mwishoni mwa wiki Yanga ilinyukwa 2-1 na Mgambo Shooting mwishoni na kuuweka rehani ubingwa wake baada ya kuachwa na Azam kwa tofauti ya pointi saba katika mbio hizo.
Katika siku za karibuni safu ya ulinzi ya Yanga imeyumba licha ya Nadir Haroub kurudi katika kiwango chake baada ya misukosuko ya muda mfupi aliyopata, pacha wake Kelvin Yondani naye ameshuka kidogo kiwango.

Kocha Pluijm aliliambia gazeti hili  kuwa mara nyingi wachezaji wake wamekuwa wakifanya makosa mengi mchezoni na wengine wakiwa hawajitolei kwa asilimia zote jambo ambalo linaigharimu timu hiyo kwa sasa.

Kocha huyo amelalamikia tabia ya wachezaji wake kutofuata maelekezo yake na kufanya tofauti na yeye anavyotaka hivyo kumpa wasiwasi kama wateweza kutetea ubingwa wao msimu huu.
“Hakuna kingine zaidi ya uzembe wetu ndio unaotugharimu, wachezaji wananiangusha hawafanyi vile ninavyotaka unawaelekeza hivi, lakini uwanjani wanafanya kitu kingine.”
“Pia tunafanya makosa mengi ambayo yanaepukika kwani makosa hayo ndiyo yanachangia timu pinzani kupata ushindi, wachezaji wanatakiwa kubadilika lazima wajitolee kisawasawa kwa ajili ya timu ili kufikia malengo yetu,”alisema Pluijm.

Aliongeza; “Siwezi kusema sasa kama bado tupo katika mbio za ubingwa au hatumo kwani wapinzani wetu wametuzidi pointi saba ni nyingi sana, kwa kuongea ni rahisi kuwa tunaweza kuwafikia kama wakipoteza baadhi ya mechi, siyo kitu rahisi, lakini tunaendelea kupambana na mwisho tutajua tuko nafasi gani kwani huu ni mpira lolote linaweza kutokea.

Pia Pluijm hakusita kuwalalamikia washambuliaji wake wakiongozwa na Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu na Jerry Tegete kwa kiasi kikubwa wamekuwa chanzo cha timu hiyo kufanya vibaya kwa sababu ya kushindwa kutumia nafasi nyingi wanazopata kufunga mabao katika baadhi ya mechi. “Katika eneo ambalo linaumiza kichwa ni la ushambuliaji, nina washambuliaji wazuri sana pengine kuliko timu yoyote kwenye ligi, lakini hawafanyi ambacho wanatakiwa kufanya, wanapata nafasi nyingi hawazitumii na kuikosesha timu ushindi.

“Wanatakiwa kubadilika na kujua wao ndio wamebeba mzigo wa timu hivyo watakiwa kufanya kazi ya uhakika ili timu ipate ushindi na pointi muhimu,” alisema.

0 Responses to “PLUIJM: WACHEZAJI YANGA WAZEMBE.”

Post a Comment

More to Read