Tuesday, April 1, 2014

RIPOTI YA CAG YAIBUA UTATA KISHERIA.




Siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kupokea taarifa kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, utata wa kisheria umegubika suala hilo kutokana na ukweli kuwa ibara ya 143 (4) ya Katiba inataka Rais aiwasilishe bungeni taarifa hiyo ndani ya siku saba.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema jana kuwa suala hilo lina madhara katika utendaji wa Serikali.

“Kuna madhara makubwa katika mzunguko wa uwajibikaji, kwani ni rahisi Serikali kuichezea taarifa ya CAG kabla haijawa ya umma. CAG anakagua fedha za Serikali kwa niaba ya wananchi kupitia Bunge. Hivyo ni lazima Bunge la Katiba lipishe Bunge la Muungano ili kupokea taarifa ya CAG,” alisema Zitto.

Aliongeza: “Tangu uhuru, taarifa ya CAG inawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa Aprili kila mwaka. Kwa hali ya sasa, Rais atakaa na taarifa hiyo kwa zaidi ya miezi miwili akisubiri Bunge kukutana.”

Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema siku hizo saba ni baada ya Bunge kuanza.

“Hakuna utata wowote hapo, ukisoma vizuri kifungu hicho kinasema, Rais atamuagiza waziri anayehusika kupeleka taarifa hiyo bungeni siku saba baada ya Bunge kuanza, siyo siku aliyokabidhiwa. Kitu muhimu hapo ni pale kikao cha Bunge kinapoanza bila kujali kinaanza lini,” alisema Balozi Sefue.

“Katika hali ya kawaida, Bunge la Bajeti lilipaswa kuanza Aprili 8. Bunge la Katiba linahitaji pesa kutoka kwenye bajeti. Sioni namna Bunge la Katiba kuendelea kwa sasa. Itabidi liahirishwe mpaka Agosti,” alisema.

Suala la kuahirisha vikao vya Bunge la Katiba kupisha Bunge la Bajeti lilielezwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyesema atamshauri Rais Kikwete kuangalia uwezekano huo.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila akizungumzia uwezekano huo, alisema Bunge hilo litasubiri ratiba ya shughuli za Bunge la Katiba.

Dk Kashilila alisema Kamati ya Uongozi wa Bunge la Katiba inatarajiwa kutoa ratiba ya shughuli zake kuelekea Bunge la Bajeti.
“Inapofika Juni, Serikali inatakiwa kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya matumizi yake, kwa hiyo mpango uliopo ni kuhakikisha kabla ya Juni 30, Bunge la Bajeti liwe limeanza kazi zake,” alisema.

0 Responses to “RIPOTI YA CAG YAIBUA UTATA KISHERIA.”

Post a Comment

More to Read