Tuesday, April 8, 2014
WAANDISHI WA HABARI WAFUNDWA KUHUSU KATIBA MPYA.
Do you like this story?
WAANDISHI wa habari wametakiwa
kuifahamu rasimu ya pili ya Katiba ili wasiipotoshe jamii wakati wa kupiga kura
ya maoni.
Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam na
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, wakati akifunga
mafunzo ya siku tatu ya masuala ya usalama kwa waandishi wa habari.
Alisema katika mchakato huo kila
kinachoandikwa kwenye vyombo vya habari wananchi wanaamini hivyo bila waandishi
kuielewa vizuri rasimu jamii itapotoshwa.
“Jamani waandishi wenzangu tuisome
vizuri rasimu hii na yale yanayopiganiwa katika Katiba… sisi ndio tutakuwa wa
kwanza kulaumiwa pindi wananchi watakapokuja kufanya uamuzi mbaya.
“Kumbukeni Katiba ni maisha ya miaka 50
ijayo hivyo kwa kuwapotosha tutaipeleka nchi pabaya… ni muhimu tukasoma na
kuelewa historia ya nchi hasa Muungano kabla ya kuandika na kutangaza kwenye
vyombo vyetu,” alisema Kibanda.
Kwa mujibu wa Kibanda, wakati suala la
muungano likiteka majadiliano ya katiba kwa sasa, suala hilo lilikuwepo siku
nyingi hata waasisi wa muungano walilijua hilo.
Amesema kutoka na elimu ndogo
iliyokuwepo awali, hata leo wanaopigania serikali tatu au mbili hawajui
matatizo gani yapo kwenye muundo wanaoutaka, hawajui itawasaidia nini na
kusisitiza kwamba waandishi ni bora warudi kwenye historia ya muungano ili
kutoa elimu sahihi kwa jamii.
Kibanda alitumia fursa hiyo kumshauri
rais atenge miaka mitano kwa ajili ya kueneza elimu ya Katiba kabla ya kuanza
mchakato wa kupata Katiba mpya.
Kuhusu usalama wa waandishi wa habari,
Kibanda alisema wanataaluma hao ni miongoni mwa makundi yanayosakawa huku
akibainisha kwamba kauli tata zinazotolewa dhidi yao hasa na viongozi wa juu
zinawafanya wanataaluma hao kudharaulika machoni mwa watu na kujengewa chuki
katika jamii.
Miongoni mwa waandishi waliohudhuria
semina hiyo ni Marine Hassan Marin, aliyesema suala la usalama kwa waandishi ni
muhimu kutolewa mara kwa mara hata katika ofisi zao.
Kwa kipindi chote cha siku tatu
walichokaa katika semina hiyo, Marin alisema amejifunza mambo mbalimbali kuhusu
kujilinda wakati wa kutafuta habari ambayo awali alikuwa hayajui.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAANDISHI WA HABARI WAFUNDWA KUHUSU KATIBA MPYA.”
Post a Comment