Tuesday, April 29, 2014
WAPINZANI WATAJA SABABU ZA KUSUSIA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MUUNGANO.
Do you like this story?
Baadhi ya viongozi wa vyama vya
upinzani wametoa sababu zilizowafanya wasihudhurie sherehe za maadhimisho ya
miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika sherehe hizo zilizofanyika
Jumamosi katika Uwanja wa Uhuru, viongozi wa vyama vikuu vya upinzani, Chadema,
CUF na NCCR-Mageuzi hawakuonekana.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa alisema kutokuonekana kwao hakuna uhusiano na msimamo wa chama wala Ukawa
kama inavyodhaniwa.
“Mwenyekiti wangu (Freeman Mbowe),
alikuwa safarini na kazi zake zote nazifanya mimi. Hata kama angekwenda
uwanjani mimi nisingekwenda kabisa,” alisema.
Alisema alishaamua kutokwenda katika
sherehe zozote za kitaifa kama maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika na Muungano
tangu mwaka 2012 kutokana na sherehe hizo kugharimu fedha nyingi ambazo
zingetumika katika maendeleo.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni
kuhusishwa na masuala ya kisiasa hususan chama tawala cha CCM.
Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu,
Habari na Uenezi (CUF), Abdul Kambaya alisema chama chake kiliamua viongozi
wote kutokuhudhuria sherehe hizo kutokana na kukosekana kwa maridhiano ya
kujadili Rasimu ya Katiba inayozungumzia muundo wa Muungano.
Alisema chama kiliona hakuna sababu ya
viongozi wake kuhudhuria sherehe za Muungano ambao majadiliano juu ya muundo
wake yameshindwa na wajumbe wa Bunge Maalumu wameng’ang’ania muundo wa serikali
mbili ambao haumo kwenye Rasimu.
“Wananchi wangetushangaa tumetoka
bungeni juzi tu hapa halafu tunahudhuria sherehe za Muungano wenye makovu,”
alisema Kambaya.
Alisema hakuna kiongozi wa chama chake aliyehudhuria
katika sherehe hizo zaidi ya Katibu Mkuu wake, Seif Sharif Hamad ambaye
alikwenda kwa shughuli za kiserikali akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena
Nyambabe alisema viongozi wa chama chake hawakuhudhuria kutokana na sababu zao
binafsi... “Hatukukaa kama chama wala Ukawa kujadili kwamba tusihudhurie
sherehe hizo,” alisema
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAPINZANI WATAJA SABABU ZA KUSUSIA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MUUNGANO.”
Post a Comment