Tuesday, April 29, 2014
UCHUNGUZI WABAINI WIZI WA MAMILIONI YA FEDHA BENKI YA BACLAYS ULIPANGWA, MAMENEJA WATIWA MBARONI.
Do you like this story?
Hatimaye Jeshi la Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam limetoa taarifa ya wizi uliotokea katika Benki ya Barclays,
Tawi la Kinondoni Aprili 15, mwaka huu, likisema tukio hilo lilipangwa ndani ya
benki hiyo.
Katika taarifa yake jana, Kamanda wa
Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema watu 13 akiwamo meneja wa tawi hilo na meneja
wake wa uendeshaji wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za wizi huo wa zaidi
jumla ya Sh500 milioni.
Kova alitoa mchanganuo wa fedha zilizoibwa
kuwa ni Sh392 milioni za Tanzania, Dola 55,OOO za Marekani, Euro 2,150 na
Paundi za Uingereza 50.
Kova aliwataja wanaoshikiliwa na polisi
kwa tuhuma hizo kuwa ni Meneja wa tawi hilo, Alune Kasililika (28), Mkazi wa
Kimara Bonyokwa na Meneja Uendeshaji, Neema Bandari.
Alisema katika wizi huo, robo tatu ya
fedha zote zilizoibwa zilichukuliwa siku moja kabla ya tukio linalodaiwa
kutengenezwa la wizi, kwa lengo la kuficha wizi huo na kwamba kulikuwa na vikao
mbalimbali vya maandalizi ya kufanikisha wizi huo.
Alisema Aprili 15, mwaka huu siku
ambayo wizi huo unatajwa kufanyika, kilichotokea ni tukio la kukamilisha njama
hizo.
“Tukio hili lilileta utata tangu mwanzo
tulipokwenda kukagua eneo la tukio, kwani siku moja kabla, yaani Aprili 14,
gari la kubebea fedha kupeleka Benki Kuu lilifika katika tawi hilo kama ilivyo
kawaida lakini fedha hazikutolewa kumbe ilikuwa ni mkakati uliowekwa
kufanikisha wizi huo.”
Alisema wachunguzi wa polisi wamebaini
kwamba fedha zilizoibwa katika benki hiyo zilichukuliwa siku moja kabla ya
tukio la kutunga.
Alisema polisi wamefanikiwa kukamata
gari moja aina ya Toyota Opa ambalo linashukiwa kutumika katika ujambazi huo na
juhudi za kutafuta gari la pili zinaendelea.
Kova alisema baadhi ya watuhumiwa
waliokamatwa na kuhojiwa walikiri kuhusika na wizi huo na walipopekuliwa
walikutwa na fedha kidogo ambazo ni sehemu ya mgawo.
“Tumegundua baadhi ya matukio ya wizi
wa fedha katika benki mbalimbali yanafanywa na wafanyakazi wa benki hizo na
matokeo yake Jeshi la Polisi linapata lawama kuwa halifanyi kazi yake kwa
ufanisi,” alisema.
Kamanda Kova aliwataja watuhumiwa
wengine wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Fredrick Lazaro (19) mkazi wa Manzese,
Kakamiye Julius (31) mkazi wa Kinondoni, Idd Nguvu (32) mkazi wa Kinondoni,
Sezary Masawe, Boniface Ndaro (29) mkazi wa Kijitonyama.
Wengine ni Erasmus Mroto (38) maarufu
kwa jina la Menyee mkazi wa Magomeni, Deo Olomy (32) mkazi wa Manzese Darajani,
Mohamed Athumani (31), mkazi wa Kimara Stopover, Joseph Mkoi (33) mkazi wa
Kimara Stopover, Lucy Amos (30) mkazi wa Tabata na Grace Amon (39) mkazi wa
Kibaha mkoani Pwani.
Katika tukio la awali, ilielezwa kuwa
majambazi hao walifika katika benki hiyo Aprili 15, mwaka huu, saa 3:00 wakiwa
na magari mawili na bunduki aina ya SMG pamoja na bastola, kisha waliingia
ndani ya benki hiyo na kupora fedha walizotoka nazo kwenye mfuko na kukimbia
nazo kwa kutumia pikipiki
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “UCHUNGUZI WABAINI WIZI WA MAMILIONI YA FEDHA BENKI YA BACLAYS ULIPANGWA, MAMENEJA WATIWA MBARONI.”
Post a Comment