Wednesday, April 2, 2014
WATANZANIA WALIOLIPULIWA NA OSAMA KUZOA SH 672BILION.
Do you like this story?
Nairobi/Dar. Watanzania wanne waliojeruhiwa katika mlipuko wa bomu
katika ubalozi wa Marekani mwaka 1998 na wengine watano waliofariki dunia
katika mlipuko huo watalipwa fidia ya Sh672 bilioni, kiwango ambacho ni sawa na
bajeti ya wizara nne za Tanzania.
Watanzania hao waliuawa na wengine kujeruhiwa
katika moja ya mashambulizi pacha yaliyotokea kwa wakati mmoja jijini Dar es
salaam na Nairobi, Kenya na ambayo yaliratibiwa na Osama Bin Laden akitumia
mtandao wa kundi la Al Qaeda mwaka 1998 kwenye ofisi za balozi za Marekani.
Katika mashambulizi hayo yaliyotokea saa 4:00
asubuhi Agosti 7, 1998, Wakenya 200, Watanzania 10 na Wamarekani 12 walipoteza
maisha na pia magaidi wawili nao walikufa.
Kati ya Watanzania 10, ni kesi za watu wanne
tu waliouawa tu zilizofunguliwa kudai fidia ya watu hao kupoteza maisha.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Marekani, Thomas
Bates alitoa hukumu hiyo wiki iliyopita, akiagiza pia kwamba serikali za Iran
na Sudan lazima zilipe jumla ya Dola za Marekani 957 milioni (Sh1.53 trilioni)
kwa Watanzania hao na Wamarekani 23 waliouawa au kujeruhiwa katika mashambulizi
pacha ya kigaidi.
Jaji Bates alisema kiasi cha Dola 488 milioni
za Marekani (Sh780.8 bilioni) kitalipwa kwa Wamarekani 12 waliouawa na familia
zao. Dola 420 milioni za Marekani (Sh672 bilioni) zitalipwa kwa Watanzania
wanne waliojeruhiwa katika mlipuko na Watanzania watano waliuawa katika
shambulio hilo. Dola milioni 49 (Sh78.4 milioni) zitalipwa kwa raia wawili wa
Marekani waliojeruhiwa katika milipuko hiyo.
“Milipuko ya mabomu katika balozi hizo mwaka
1998 iliwaathiri wanaoshtaki katika kesi hii, “Jaji Bates aliandika. Kupitia
simulizi zao binafsi, inaonyesha kwamba hata zaidi ya miaka 15 baadaye kila
mmoja bado ana kumbukumbu za kutisha za siku hiyo.
“Fidia hii haiwezi ikarudisha maisha ya wale
waliokufa wala waliopata madhara. Badala yake, ni ya kutoa tu kifuta machozi.
Lakini hiyo ni kidogo sana kwa wale wanaoshtaki.”
Hata hivyo, uamuzi wa Jaji Thomas Bates
haujaeleza fedha hizo zitalipwa lini kwa waathirika hao.
Kiwango cha Sh672 bilioni ni sawa na bajeti
za Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo katika mwaka wa fedha wa
2013/14 ilitengewa Sh20.4 bilioni, Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (Sh21.3
bilioni), Uchukuzi (Sh491.1 bilioni ) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa iliyotengewa Sh138.3 bilioni.
Thomas Fay, wakili aliyewawakilisha
Watanzania na Wamarekani, alisema kuwa juhudi zinazotakiwa sasa ni kuanza
kutambua mali za Iran na Sudan ambazo zinaweza kutaifishwa ili kulipa fidia
hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa Washington alisema kuwa
hukumu ya Jaji Bates ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa Wamarekani na
Watanzania walioathirika kwa ugaidi huo wanapata haki kwa mateso waliyoyapata.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WATANZANIA WALIOLIPULIWA NA OSAMA KUZOA SH 672BILION.”
Post a Comment