Thursday, May 1, 2014
BAJETI KUU YA SERIKALI ;TAKRIBANI SH. TRI. 19.7 ZATARAJIWA KUTUMIKA MWAKA 2014/2015.
Do you like this story?
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda akizungumza na wabunge wakati wa kupokea taarifa ya Wizara ya fedha jijini Dar es salaam. |
Serikali imepanga
kutumia jumla ya sh.19, 653.31 ambayo ndiyo sura ya bajeti katika mwaka wa
fedha 2014/2015 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo ya nchi na
watu wake.
Kauli hiyo
imetolewa na Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum alipokuwa akiwasilisha taarifa
ya sura ya Bajeti kuu ya Serikali inayotarajia kuanza kutumika mwaka wa fedha
unaoanza Julai 2014/2015 leo (jana) jijini Dar es salaam.
Waziri Saada alisema
kuwa mfumo wa bajeti kwa mwaka wa fedha unaoanza unazingatia sera za bajeti kwa
mwaka 2014/2015 ambazo zitazingatia vipaumbele vya mpango wa Maendeleo wa
Taifa na malengo ya utekelezaji wa mkakati wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Kwa upande wa
matumizi ya kawaida Serikali inatrajia kutumia jumla ya sh.trilioni 14, 208. 21
ambayo inajumuisha mfuko mkuu wa serikali, mishahara ya watumishi wa Serikali,
wizara, mikoa, halmashauri, taasisi na wakala za Serikali.
Aidha, kwa matumizi
mengine yatakuwa ni kwa ajili ya maendeleo kwa mwaka wa fedha unaotarrajiwa
kuanza Julai mwaka huu ambapo kiasi cha 5, 445.10 ambazo ni sawa na asilimia
27.7 zimepangwa kutumika kwa kuhusisha fedha za ndani na za nje ya nchi.
Waziri Saada
akiwasilisha taarifa yake kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, wabunge hao waliipokea Taarifa ya Serikali kuhusu Makadirio ya Bajeti
katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam ambayo
inatarajiwa kuongeza wigo wa wabunge kuijadili bajeti hiyo kabla ya kusomwa
bungeni mjini Dodoma.
Shabaha ya bajeti ya
mwaka ujao wa fedha ni kuhakikisha pato la taifa litakuwa kwa asilimia 7.2
mwaka 2014, asilimia 7.4 mwaka 2015, asilimia 7.7 mwaka 2016 na kuendelea
kuongezeka hadi kufikia asilimias 8.0 ifikapo mwaka 2017.
Misingi ya bajeti ya
Serikali kwa kipindi cha mwaka 2014/2015 ni pamoja na kuendelea kuwepo na
kuimarishwa amani, usalama, utulivu na utengamano misingi ambayo itasaidia
kupatikana kwa katiba mpya kwa wakati kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake
Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu Stephen Wasira akiwasilisha
rasimu ya mpango wa maendeleo wa taifa katika bunge likikaa kama kamati alisema
kuwa maeneo ya vipaumbele yanalenga miradi ya kitaifa ya kimkakati
inayolenga kutanzua vikwazo vikuu vya kiuchumi inajumuisha miundombinu ya
uasfirishaji kama reli, barabara, bandari, na usafiri wa anga.
Vipaumbele vingine ni
nishati, huduma ya maji mijini na vijijini, kilimo, viwanda, maendeleo ya
rasilimali watu na huduma za kiuchumi kama fedha, biashsra na utalii.
Naye Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amewaasa wabunge
wote washiriki kikamilifu katika kamati pamoja na serikali ili ipatikane bajeti
yenye tija kwa taifa na wabunge waikamilishe kizalendo kwa kujali nchi
yao.
Kikao cha Bunge la
bajeti kinatanguliwa na kamati mbalimbali zitakutana ambapo vikao vilianza
Aprili 27, 2014 kwa wajumbe kuwasili jijini Dar es salaam na kuhitimishwa Mei 4,
2014 na wabunge kuanza safari kwenda Dodoma tayari kwa kuanza kikao chake kama
ilivyopangwa.
Kamati ya bunge ya
Kilimo, Mifugo na Maji, kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira wakati wa Bunge la bajeti, kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu,
kamati ya Nishati na Madini, kamati ya Bunge ya hesabu za Serikali (PAC)
kujadili hesabu zilizokaguliwa za Serikali kuu na mashirika ya umma, kamati ya
kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Na nyingine ni kamati
ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala, kamati ya kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, kamati
ya kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI, kamati ya LAAC Dar es salaam na kamati
ya kudumu ya bunge ya maendeleo ya jamii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BAJETI KUU YA SERIKALI ;TAKRIBANI SH. TRI. 19.7 ZATARAJIWA KUTUMIKA MWAKA 2014/2015.”
Post a Comment