Friday, May 23, 2014

EMMANUEL ANORD OKWI ALAMBA MILIONI 10 KWA SAA YANGA.




STRAIKA, Emmanuel Okwi ameichezea Yanga dakika 687 kwenye mechi nane kwa msimu ulioisha na kuzoa kitita cha Sh120 Milioni sawa Sh 10 Milioni kwa kila saa moja aliyochezea klabu hiyo ya Jangwani ndani ya jezi namba 25.

Fungu hilo linahusisha mishahara na dau la usajili.  Katika miezi hiyo minne, amefunga mabao matatu tu.
Lakini mabao hayo hayakuwa na madhara chanya kwa Yanga kwani mawili alifunga Yanga ikiwa imeshinda mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Ligi na moja aliifunga Simba iliposhinda mabao 3-1 kwenye Mtani Jembe.

Mabao ya mchezaji huyo ambaye imeanza kudaiwa kwamba anafikiria kuvunja mkataba na Yanga kutokana na ushawishi wa wagombea wa Simba hayakuipa Yanga faida yoyote zaidi ya kuongeza idadi.

Okwi ambaye sasa yupo katika mgogoro na Yanga akitaka amaliziwe fedha zake za usajili, ameichezea klabu yake mechi hizo huku akikosa nyingine saba kwa sababu mbalimbali ikiwemo kugoma na kukosa kibali.

Nyota huyo aliyeanza kibarua chake Yanga mwishoni mwa mwaka jana baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na nusu, ameichezea Yanga kwa dakika 687 (Sawa na michezo nane) ambazo ni mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika lakini akaunti yake ikafurika Sh120 Milioni.

Kati ya Sh120 Milioni alizolipwa Okwi, Sh 96 Milioni alilipwa kama sehemu ya ada yake ya usajili alipojiunga na Yanga lakini Sh. 24 Milioni alilipwa kama mshahara wake kwa miezi minne aliyocheza kabla ya kugoma akishinikiza kumaliziwa kulipwa fedha zake za usajili.

Kwa mwezi Okwi analipwa dola 4,000 ambazo ni zaidi ya Sh. 6 Milioni hivyo kwa miezi minne alilipwa Sh. 24 milioni. Okwi alisajiliwa kwa dau la dola 100,000 ambazo ni zaidi ya Sh. 160 Milioni, lakini Yanga ilimlipa kianzio cha dola 60,000 (Sh96 Milioni) hivyo sasa anaidai dola 40,000 zilizobaki.

Mechi alizoichezea Yanga ni sita za ligi kuu ambazo ni dhidi ya Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar, Azam FC, Rhino Rangers, Prisons (hakucheza dakika zote tisini) na Mgambo JKT, wakati kwa upande wa michezo ya kimataifa amecheza mechi mbili nyumbani na ugenini dhidi ya  Al Ahly ya Misri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kutokana na kibali chake kuchelewa kuwasili nchini, Okwi alikosa mechi tatu za mwanzo za mzunguko wa pili wa ligi kuu ambazo ni dhidi ya Ashanti United, Coastal Union na Mbeya City. Mechi nyingine aliokosa Okwi ni dhidi ya Komorozine de Domoni ya Comoro iliyokuwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia straika huyo aligomea michezo ya mwisho ya ligi hiyo dhidi ya Simba, JKT Oljoro, JKT Ruvu na Kagera Sugar.
Ukiachana na mechi hizo nane za michuano mbalimbali, Okwi aliichezea Yanga mechi ya kwanza dhidi ya Simba Desemba mwaka jana mchezo maalumu wa kirafiki uliopewa jina la Nani Mtani Jembe, pia alicheza mechi nne za kirafiki walipokuwa kambini Uturuki.

Rekodi zinaonesha kuwa tangu Okwi aondoke Simba mwaka 2012, amecheza jumla ya michezo 14 tu za kimichuano kwenye nchi tatu tofauti za Tunisia, Uganda na Tanzania. Aliichezea mechi mbili Etoile Du Sahel ya Tunisia, akacheza nne Uganda akiwa na SC Villa na nane akiwa na Yanga.

Akiwa Tunisia Okwi aliichezea mechi mbili Sahel akitokea benchi lakini hakuweza kuwa na maisha mazuri kwani aliachana na timu hiyo na kutimkia Uganda alipocheza mechi nne za Ligi Kuu ya Uganda baada ya kutokea matatizo ya malipo yake.

Kwa sasa Okwi yupo Uganda huku majaliwa yake katika kikosi cha Yanga yakiwa shakani kwani mwenyewe anadai amaliziwe fedha zake za usajili lakini uongozi unamtaka ajieleze kwa nini amegoma kuichezea timu hivyo unapanga kumkata sehemu ya fedha zake za usajili.

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji (pichani) amesisitiza kwamba kwavile mchezaji huyo haikutumikia Yanga ipasavyo lazima wakae mezani wajadiliane mambo mawili aongeze mkataba mpaka kufikia miaka mitatu au wamkate kiasi cha fedha anazoidai.

Lakini mwanasheria wake, Edgar Aggaba amejibu kwamba hakuna kitu kama hicho, Manji anapaswa kulipa dau walilokubaliana halafu wakae mezani wazungumze mengine.
 Chanzo: Mwanaspoti

0 Responses to “EMMANUEL ANORD OKWI ALAMBA MILIONI 10 KWA SAA YANGA.”

Post a Comment

More to Read