Saturday, May 24, 2014
JICHO LANGU LA TATU: REAL MADRID v ATLETICO MADRID
Do you like this story?
Leo, ndiyo siku ya hukumu! Katika
uwanja wa Estadio da Luiz, jijini, Lisbon, Ureno wakati miamba ya soka nchini
Hispania itakapokuwa ikiwania taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Ni fainali
ya kwanza baada ya miaka 14 timu za Hispania kukutana katika mchezo wa fainali
wa michuano hiyo mikubwa na yenye mvuto mkubwa barani ulaya kwa ngazi ya klabu.
Real, iliichapa Valencia kwa magoli 3-0, mwaka 2000 katika fainali ya mwisho
kuhusisha klabu za Hispania.
Atletico, kwa upande wao wamekuwa na
msimu wa kuvutia. Wametwaa taji la LaLiga, wiki iliyopita, na wanaweza kutwaa
taji lao la pili kubwa msimu huu kama watafunga ' msimu wa ulaya' kwa kuwanyuka
mahasimu wao wa jiji la Madrid, usiku wa leo.
Bjorn Kuipers, raia huyu wa Uholanzi
mwenye miaka 41 atachezesha pambano hilo ambalo kwa mara ya kwanza litahusisha
timu za mji mmoja, akiwa na rekodi ya kutoa kadi nyekundu mbili, na njano 16
katika michezo tofauti aliyocheza msimu katika michuano, Kuipers itambidi kuwa
ngangari kuchezesha wachezaji ' wababe-wachapa viatu' wa timu zote mbili. XABI
ALONSO kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania hatakuwepo katika mchezo wa leo,
hivyo kocha, Carlo Ancelotti anataraji kumuanzisha kiungo, Mjerumani, Sami
Khedira ambaye alicheza kwa nusu ya mchezo wa mwisho wa timu yake katika ligi
kuu.
Alonso, alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi
cha Real, atakosa mchezo huo kwa kuwa anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano
ambazo alizipata katika michezo ya nusu fainali dhidi ya Bayern Munich.
Luka Modric na Angel Di Maria
wanataraji kuanza na Khedira na kikosi hicho cha ' watu watatu' kinaweza
kujikuta katika wakati mgumu dhidi ya timu ya Diego Simeone ambayo imekuwa
ikiwachezesha viungo wa nne hadi watano katikati ya uwanja. Koke, Thiago
Mendes, ArdaTuran, ni wachezaji wagumu uwanjani, wanakaba kwa nguvu hadi hatua
ya mwisho, wanachezesha timu na kuzuia kwa pamoja, na siri kubwa ya mafanikio
ya timu hiyo msimu huu ni kucheza kwa ushirikiano, huku wachezaji wote wakiwa
na majukumu sawa. Ni tofauti na Real ambayo imekuwa timu inayotegemea zaidi
uwepo wa Cristiano Ronaldo na kiwango cha Mreno huyo katika mchezo wa leo
ndicho kinaweza kuamua kama mabingwa hao mara tisa wa kihistoria kutwaa ubingwa
wao wa kwanza baada ya miaka 11.
Katika muda wa miaka miwili, timu hizo
zimekutana mara sita katika michuano tofauti. Real iliifunga, Atletico kwa
magoli 2-1 , april, mwaka jana katika uwanja wa Vicente Calderon, na mara ya
mwisho kwa kikosi cha Simeone kuwashinda mahasimu wao ni katika mchezo wa kwanza
wa msimu uliomalizika, mwezi, septemba walipoilaza, Real kwa goli 1-0, pale
Santiago Bernabeu.
Timu hizo zimekutana mara nne msimu huu.
Tarehe 5, februari, Real iliichapa, Atletico kwa magoli 3-0 katika nusu fainali
ya Copa del Rey, na wakawatandika tena
magoli 2-0 katika nusu fainali ya pili na kutinga fainali ambayo walitwaa
ubingwa. Atletico haijaifunga, Real katika michezo mitatu ya mwisho walipoteza
mchezo mmoja na kulazimisha suluhu mchezo mmoja katika michezo miwili ya La
Liga. Hivyo, Real wanaweza kujiamini kupita kiasi na kujikuta wakishindwa
kutimiza lengo la kutwaa, ' La Decima'.
Kufikia hatua ya fainali, Atletico
haijapoteza mchezo wowote kati ya 12 waliyocheza katika michuano hiyo msimu
huu, wakati Real walipoteza dhidi ya Borussia Dortimund kwa magoli 2-0 katika
mchezo wa pili wa hatua ya robo fainali ambao nyota wake, C. Ronaldo hakuwepo
uwanjani. Kikosi cha Simeone kimefunga magoli manne tu dhidi ya mahasimu wao wa
Madrid katika michezo sita ya mwisho wakati Real imetikisa nyavu za wapinzani
wao mara tisa. Kitu kinaweza kutokea leo? Inaweza kuwa fainali nzuri na yenye
magoli mengi kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita wakati timu za FC Port na AS
Monaco zilipocheza fainali‘
isiyotarajiwa’na Monaco walilala kwa
magoli 3-0, au inaweza kuwa fainali ngumu
na ya kuvutia kama ile ya Mocsow, 2008 wakati mshindi alipopatikana
baada ya dakika 120 kwa timu za England, Manchester United na Chelsea kukutana
fainali, au inaweza kuwa fainali ya kusisimua kama ile ya Liverpool na AC
Milan, 2005.
Hii ni mechi ya fainali, hivyo si
rahisi kutabiri mshindi wake. Atletico wanashambulia kuanzia nyuma huku
wakisogea mbele kwa uangalifu mkubwa, hawafunguki sana uwanjani dhidi ya timu
kali na hiyo ndiyo imekuwa sababu ya wao kuzishinda, FC Barcelona na Chelsea
katika hatua za robo na nusu fainali. Walifunguka dhidi ya Milan na waliweza
kuitoa timu hiyo ya Italia kwa jumla ya magoli 4-1 Katika hatua ya 16, lakini
kukutana kwao na ‘ BBC’ iliyo katika mwendo kasi inaweza kuwa tabu kwao.
Walifungwa magoli matano katika michezo miwili ya robo fainali mwezi February
katika kombe la Mfalme ila bado silaha yao muhimu‘ ya kujilinda’ inaweza
kuwasaidia kunyanyua kikombe cha nne cha ulaya ndani ya miaka minne.
Washindi hao wa ligi ya ulaya miaka ya
2010 na 2012, na taji la Uefa Super Cup
wamekuwa na mafanikio makubwa katika michuano ya ulaya katika miaka ya
karibuni, tofauti na wapinzani wao ambao wamefuzu fainali ya kwanza baada ya
miaka 11. Real iliifunga, Bayer 04 Leverkusen ya Ujerumani katika mchezo wa
fainali mwaka 2002 na timu imefuzu fainali msimu huu baada ya kukwama mara tatu
mfululizo katika hatua ya nusu fainali. Tamaa yao ya ubingwa wa‘ kumi’ inaweza
kumalizwa na timu inayosaka taji la kwanza
usiku wa leo.
Real humaliza mechi kwa kushambulia kwa
kasi ikitokea kulia mwa uwanja, upande wa kushoto na wakati mwingi
wakishambulia na kufunga wakitokea katikati ya uwanja. Gareth Bale, alifunga
goli la ‘ ajabu’katika mchezo wa fainali wa kombe la mfalme dhidi ya Barcelona,
machi mwaka huu, kocha, Carlo humtumia mchezaji huyo katika kuvuruga mbinu za
kijilinda za mabeki wa timu pinzani kitu ambacho kimekuwa na mafanikio makubwa
hata dhidi ya wapinzani wao wa mchezo wa leo. Karimu Benzema amekuwa mfungaji‘
huru’na mchezaji anayefunga magoli muhimu. Wakati, Ronaldo ni silaha ya hatari
katika mashambulizi ya kushtukiza. Je, mbinu hiyo inaweza kufanya kazi katika
mchezo wa leo?
Kama, Atletico watapata goli la mapema,
mechi inaweza kuwa ngumu kwa Real, na endapo Real wataanza kufunga mambo
yanaweza kugeuka na kuwa fainali ya magoli mengi. Atletico huwa wakicheza kwa
kujihami sana mara wanapopata goli la kuongoza,
kitu ambacho kimekuwa na mafanikio makubwa kutokana na wachezaji wote
kucheza kwa lengo la kulinda ushindi. Ni vigumu kusawazisha goli dhidi ya timu
hiyo, ila wana uwezo wa kurudi uwanjani na kufuta matokeo mabaya wanapokuwa
nyuma dhidi ya wapinzani wao. Fainali haina mwenyewe, ila kuna historia itaandi
kwa leo, iwe ni kwa upande wa makocha au klabu. Simeone anasaka taji lake la
kwanza wakati, Carlo anasaka taji la tatu kiufundishaji. Real wanasaka taji la
kumi‘ La Decima’ wakati Atletico wanasaka taji la kwanza la mabingwa wa Ulaya. Nani mshindi? Mimi sijui!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “JICHO LANGU LA TATU: REAL MADRID v ATLETICO MADRID”
Post a Comment